Na Mwandishi Wetu, JamhuriMwdia, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Bodi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari amewapongeza waandishi wa habari kwa kuhamasika, kuandika kwa umahiri na weledi kisha kusambaza taarifa za hali ya hewa.
Jaji Bakari alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akikabidhi tuzo na zawadi kwa waandishi vinara wa habari za hali ya hewa kwa mwaka 2023/2024 huku akieleza namba TMA inavyothamini tasnia ya habari kwa kuongeza wigo wa washindi na zawadi.
“Lengo kuu la Tuzo hizi ni kuendelea kuleta hamasa na kuongeza umahiri wa uandaaji na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa jamii, na kuimarisha mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa,” alisema Jaji Bakari.
Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema TMA ni moja ya taasisi chache nchini zinazothamini mchango wa wanahabari kwa ujumla ikiwemo ubunifu wa kuanzisha tuzo za waandishi wa habari bora za hali ya hewa nchini kwa miaka mitano sasa.
“Katika kuhakikisha tuzo hizi zinaendelea kuwa bora zaidi, mwaka huu Mamlaka imeboresha maeneo kadhaa ikiwemo kuongeza vipengele viwili vya waandishi kutoka nje ya Dar es Salaam na Zanzibar na kuboresha zawadi za washindi, hongereni sana TMA,” alisema Jaji Bakari.
Akimkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA, Dk. Hamza Kabelwa, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri alisema Mamlaka kwa kutambua mchango wa vyombo vya habari na kuahidi kuendelea kushirikiana nao.
“Kuonesha namna tunavyothamini na kushirikiana na waandishi wa habari, TMA imewezesha baadhi yao kimafunzo ndani na nje ya nchi kwa vipindi tofauti kwa miaka 15 sasa hususani kipindi cha maandalizi ya utabiri wa mvua za misimu,” alisema Dk. Kabelwa.
Washindi wa tuzo za umahiri wa habari mwaka 2023/2024 ni John Mathias kutoka TBC1; Othman Ali Juma kutoka gazeti la Alnoor Zanzibar na Lionel Ernest kutoka gazeti la Uhuru.
Wengine ni Adam Hando kutoka redio CGFM kutoka Tabora na Zaituni Mkwama kutoka Daily news Online.
Akizungumza kabla ya kuanza kutolewa kwa kwa tuzo hizo, Kaimu Meneja wa Masoko na Mawasiliano ya TMA, Monica Mutoni alisema jumla ya kazi 115 ziliwasilishwa kutoka kwa waandishi 38 hapa nchini.
“Tunaendelea kuwahamasisha waandishi wa habari kutuma kazi zao kwenye email yetu naomba mzingatie tunapotangaza kuanza kupokea habari za tuzo,” alisema Mutoni.