Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ,imesema kutakuwa na ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo nchini hali ambayo imesababisha kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtaalamu wa hali ya hewa TMA, Joyce Makwata amesema vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi Novemba, 2022 na upungufu wa mvua na kupungua kidogo ifikapo mwezi Desemba,2022.
Amesema kuwa kutokana na hali hiyo kumekuwepo kwa ongezeko la joto katika maeneo mbalimbali nchini hali iliyosababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi nchini kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
“Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa), Jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine,” amesema mtaalamu huyo.
Amesema kuwa katika kipindi cha Oktoba, 2022, hali ya joto iliongezeka katika maeneo mbalimbali nchini kwa kiwango cha juu zaidi cha joto cha nyuzi joto 36.9 0C kiliripotiwa katika kituo cha Mpanda, Katavi mnamo Oktoba 26, 2022.
“Kiwango hiki ni sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.0 0C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa Oktoba, huku baadhi ya maeneo mengine yaliyokuwa na ongezeko la joto kwa Oktoba, 2022 ni pamoja na Mkoa wa Tabora nyuzi joto 35.7 (ongezeko la nyuzi joto 3.0), Moshi nyuzi joto 34.1 (ongezeko la nyuzi joto 3.2) na Dar es Salaam nyuzi joto 32.8 (ongezeko la nyuzi joto 1.4),” amesema.
Aidha,katika wiki mbili za mwanzo za Novemba, 2022; hali ya ongezeko la joto iliendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo ambapo kituo cha Mpanda kiliripoti nyuzi joto 35.4 0C mnamo tarehe 2 Novemba, 2022 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.7 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba.
“Kituo cha Tabora kiliripoti nyuzi joto 34.8 (ongezeko la nyuzi joto 3.7), Dar es Salaam nyuzi joto 33.7 (ongezeko la nyuzi joto 2.1) pamoja na Kilimanjaro nyuzi joto 34.3 (ongezeko la nyuzi joto 2.4),” amesema.
Ilisema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kuepuka au kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo ongezeko la joto.