Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kufatilia taarifa za hali ya hewa ili kuongeza tija katika shughuli zao.

Aidha amesema kuwa Mamlaka hiyo hivi karibuni itatoa taarifa za msimu wa Vuli ambapo itaeleza kwa kina nini matarajio yao katika msimu huo.

Ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane-Nzuguni jijini Dodoma.

“Katika muktadha huu ambapo Dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, wananchi wote tunapaswa kuendelea kufatilia kwa umakini zaidi taarifa za hali ya hewa za kila siku, kila mwezi, kila msimu ili kuweza kuongeza tija na ufanisi kwenye shughuli zetu lakini tuweze kuepuka hasara ambayo inatokana na kutokutumia taarifa za hali ya hewa lakini kubwa zaidi kuendelea kuokoa maisha ya watu na mali zao kutokana na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa.

” Na hivi karibuni tutatoa taarifa za msimu wa Vuli ambapo tutaweza kuwaeleza kwa kina nini matarajio yetu katika msimu ujao wa Vuli. Kwahiyo tunaomba wananchi wajiandae kusikiliza na kufatilia na kuzitumia hizo taarifa kwaajili ya maendeleo endelevu ya taarifa hizo,” amesema.

Aidha ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kufatilia na kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa namba 2 ya Mwaka 2019 ambayo inatoa maelekezo mbalimbali kwa kila Mwananchi na kutumia hizo taarifa.

“Pia kwa wale ambao wana vifaa vya hali ya hewa wahakikishe vifaa hivyo vimesajiliwa na TMA na pia vinakidhi vigezo ambavyo vinahitaji kwa upande wa nchi na kimataifa,” amesisisitiza.

Akizungumzia ushiriki wao katika maonesho hayo, amesema wameweza kutoa elimu ya matumizi sahihi ya huduma za Hali ya Hewa pamoja na kuendelea kuwasisitiza wananchi na jamii kwa ujumla kuendelea kufatilia kwa makini na kuzingatia taarifa zinazotolewa na TMA hususani taarifa za utabiri wa msimu, utabiri wa kila siku 10, kila mwezi na utabiri wa kila siku.

“Taarifa hizi zinakuwa na tija kubwa na zinachangia katika kuongeza tija na ufanisi katika shughuli mbalimbali za Kilimo, viwanda, ujenzi, usafiri wa anga, nchi kavu na majini. Kwa ujumla taarifa zetu ni taarifa ambazo tunazitoa zinatumika na sekta zote pamoja na wananchi,” amesema.

Amesema kuwa katika maonesho hayo, wametembelewa na wanafunzi kutoka shule za Msingi, sekondari, vyuo mbalimbali, na wengi wao wakitaka kupata elimu zaidi ya hali ya hewa na mabadiliko yake.

“Ambapo wataalamu bingwa katika banda letu wameendelea kutoa hiyo elimu. Lakini kwa Wakulima na Wafugaji wameendelea kutembelea na kutaka kupata taarifa kuhusiana ni namna gani ambavyo wanaweza wakazitumia vizuri katika kuongeza tija na ufanisi kwenye shughuli zao.

“Lakini pia tumetembelewa na watafiti, wajenzi ambapo pia wanataka kupata kwa kina taarifa hizi tunazozitoa lakini pia wakiwa na maswali kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea sasa hivi,” amefafanua.