Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga ‘CHIDO’ katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar.
Taarifa iliyotolewa jana na Mamlaka hiyo,imesema mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya
kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku nne zijazo kuanzia Disemba 13 hadi 16, 2024.
Amesema kuwa kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja nchini.”Kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO”kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo jirani hususan kati Disemba 14 na 16 ya Disemba 2024,”amesema.
Aidha imetoa ushauri kwa watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
TMA imesema itaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.