Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kumekuwepo na ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo nchini hususan yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka kwa miezi ya hivi karibuni.
Hali hii imesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo hayo.
Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine.
Katika kipindi cha mwezi Februari, 2025 hali ya ongezeko la joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo hadi kufikia tarehe 11 Februari, 2025 kituo cha hali ya hewa cha Mlingano (Tanga) kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 36.0°C mnamo tarehe 05 Februari ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 2.1°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Februari.
Kituo cha hali ya hewa kilichopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kiliripoti kiwango cha juu cha nyuzi joto 35.0°C mnamo tarehe 10 Februari, 2025 (ongezeko la nyuzi joto 2.2°C). Kituo cha Tanga kiliripoti nyuzi joto 35.1°C mnamo tarehe 10 Februari (ongezeko la nyuzi joto 2.3°C), Kibaha nyuzi joto 35.8 °C mnamo tarehe 10 Februari (ongezeko la nyuzi joto 3.0°C), na Kilimanjaro nyuzi joto 34.3°C mnamo tarehe 09 Februari, 2025 (ongezeko la nyuzi joto 0.6°C).
Aidha, ongezeko la unyevu angani (Relative humidity) katika kipindi hiki linalosababishwa na mvuke wa bahari hususan katika maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo jirani limechangia pia mwili kuhisi joto zaidi ya viwango vinavyoripotiwa.
Vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi huu wa Februari, 2025 hususan katika maeneo ambayo msimu wa mvua za Vuli umeisha.