Dar es Salaam, 22 Mei 2024 Saa 4 Usiku:
Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa za kilichokuwa Kimbunga “IALY” zilizokuwa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu tarehe 17 Mei 2024.
Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha saa 6 zilizopita, Kimbunga “IALY” kimepoteza kabisa nguvu yake, kikiwa kaskazini mashariki mwa pwani ya Kenya.
Hivyo, kwa sasa hakuna tena tishio la kimbunga “IALY” katika nchi yetu. Aidha, wakati kikipita karibu na pwani na nchi yetu kati ya jana tarehe 21 na leo tarehe 22 Mei 2024 kimeweza kusababisha vipindi vya mvua, upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo ya pwani ya nchi yetu kama ilivyotabiriwa awali.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa, japo tunaelekea mwishoni mwa msimu wa Masika, 2024, tunakaribia kuanza kwa msimu wa Kipupwe, na kwas ababu hiyo, vipindi vya upepo wa Kusi baharini vinaweza kuanza kujitokeza na kuambatana na mawimbi makubwa kwa baadhi ya nyakati.
USHAURI: Wananchi na watumiaji wa bahari wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika.
Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania