Dar es Salaam, 04 Mei 2024 Saa 5:59 Usiku:
Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa za kilichokuwa Kimbunga “HIDAYA” zilizokuwa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu tarehe 01 Mei 2024.
Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha masaa 6 yaliyopita, Kimbunga “HIDAYA” kimepoteza kabisa nguvu yake baada ya kuingia nchi kavu katika kisiwa cha Mafia.
Aidha, mabaki ya mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yalisambaa katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa kusini mwa nchi yetu hususan katika maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro na maeneo jirani. Hivyo, hakuna tena tishio la kimbunga “HIDAYA” katika nchi yetu.
Hata hivyo, vipindi vya mvua za kawaida za Masika zinatarajiwa kuendelea katika baadhi ya maeneo hasa ya ukanda wa ziwa Victoria, Nyanda za Juu kaskazini-mashariki na ukanda wa pwani ya kaskazini.
USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika.
Imetolewa na: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.