Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), kimelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha mtuhumiwa mkuu aliyesababisha tukio la kubakwa na kulawitiwa kwa binti wa Yombo anafikishwa mahakamani upesi ili haki ipatikane.

Akizungumza na vyombo vya habari rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, amesema ni muhimu kwa sheria kuchukua mkondo wake bila kuchelewa.

“Tunataka na aliyesababisha kitendo kile kufanyika na yeye ni mkosaji, afikishwe mahakamani mara moja, TLS itaona namna bora ya kuweka wakili atayekua aki-watchbrief (akijulisha kinachoendelea) ili kuona maendeleo ya shauri lile yatakavyokuwa yakiendelea na kuhakikisha haki za binti yule hazipotei,” amesema Mwabukusi

Hadi sasa Jeshi la Polisi limewafikisha mahakamani washtakiwa wanne kati ya sita waliohusika katika tukio la ukatili wa kijinsia walioonekana kwenye video wakidai kuwa ‘wametumwa na afande’, jambo ambalo limezua maswali mengi kutoka kwa umma kuhusu nani anayeweza kuwa mhusika mkuu wa tukio hilo.

Washtakiwa wanne waliofikishwa Mahakama ya Hakimu mkazi Dodoma jana Agosti 19 ni askari wa JWTZ Clinton Damas, askari Magereza Praygod Mushi, Lord Lema na Nickson Jackson.

Hata hivyo, washtakiwa wote wamekana mashtaka yanayowakabili na kesi hiyo itaendelea kuunguruma kwa wiki nzima hadi ijumaa Agosti 23,2024.

Aliyekuwa mgombea uraisi wa chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS)Boniface Mwabukusi akizungumza na waandishi wa nhabari kupinga hatua ya yeye kuenguliwa katika nafasi ya kugombea.Picha na Michaelk Matemanga

Awali TLS ilitoa tamko kulaani kitendo hicho cha udhalilishaji na ukatili wa kijinsia alichofanyiwa binti huyo na washtakiwa ambao wawili wamebainika kuwa ni askari wa vyombo vya usalama nchini.

Aidha, TLS imetoa wito kwa Jeshi la Polisi kuimarisha madawati ya jinsia kwenye chombo hicho ili kiweze kushughulikia changamoto za ukatili wa kijinsia kwa ufasaha.

“Waimarishe madawati ya kijinsia ili kuweza kushughulikia changamoto za ukatili wa kijinsia, isiwe madawati kama jina, iwe ni sehemu ambayo kuna watu wanachukia vitendo hivi, wenye uweledi wa kukabiliana na madhira haya” amesema Mwabukusi.

Tukio hili limeibua hisia kali miongoni mwa wananchi na mashirika ya haki za binadamu, wakitaka hatua za kisheria zichukuliwe haraka ili kutoa fundisho kwa wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) ameonesha wasiwasi juu wa jinsi Jeshi la Polisi linavyoshughulikia suala hilo, akisema kwamba Polisi siyo mahali salama kwa binti huyo, na kwamba kuna uwezekano wa kuteseka zaidi kisaikolojia ikiwa ataendelea kuwa mikononi mwao.

Zitto amezitaka taasisi za haki za binadamu kama Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) kumchukua binti huyo kutoka mikononi mwa Polisi na kumweka chini ya uangalizi wao kwa kuwa ni hatari kwa binti huyo kuendelea kubaki chini ya uangalizi wa Polisi, akihofia kuwa badala ya kupata msaada, huenda akapata mateso zaidi.