Walau sasa sura ya utaifa katika Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza kuonekana, kutokana na kila kanda kuwakilisha timu zao kutoka kwenye mikoa husika.
Katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, ni minane tu yenye timu zinazoshiriki Ligi Kuu, mingi ikiwa na timu zaidi ya moja.
Dar es Salaam ina timu tano, Mbeya ina timu mbili, Shinyanga
inawakilishwa na timu mbili, Mwanza ina timu mbili, Ruvuma,
Morogoro, Pwani na Kagera ina timu moja moja kila moja.
Ajabu, kuna baadhi ya mikoa inayosifika kwa kutoa vipaji vya soka au iliwahi kuwa na timu tishio katika miaka ya 1980, 1990 na 2000
mwanzoni lakini sasa haina kitu.
Hali hiyo huenda inatokana na matatizo ya ubinafsi wa watu, kutojituma na ikiwezekana viongozi kutokuwa wabunifu au kukosa mapenzi ya dhati na mchezo huo.
Mikoa hii ilikuwa na timu tishio ambazo zilikuwa moto wa kuotea mbali kiasi cha klabu kongwe za Simba na Yanga zilikuwa zikipata shida kupata matokeo.
Lakini leo hizi timu zimekufa ama nyingine zipo lakini zinashindwa
kupata fursa ya kurudi Ligi Kuu Bara, kutokana na matatizo mbali mbali.
Hivyo basi, leo tuangalie timu za mikoa mbalimbali zilizotesa lakini leo zimepotea na nyingine zimeshakufa na kubaki historia. Pamba au TP Lindanda Wana Kawekamo (Mwanza)
Mwanza ilipewa jina la Brazil ya Tanzania na hiyo ilitokana na rundo la vipaji ndani ya mkoa huo ambao umewahi kutikisa vilivyo na klabu ya Pamba au TP Lindanda. Lakini ilikuja kupotea na stori ikawa ni Toto African.
Pamba ilikuwa tishio enzi zake, ilikuwa ni timu ambayo haikubali
kufungwa katika uwanja wake wa nyumbani wa CCM Kirumba, na ilikuwa inakonga nyoyo za wana-Mwanza.
Enzi hizo Pamba ilizalisha wachezaji wengi mahiri kama akina Ibrahim Magongo, Deo Mkuki, Fumo Felician, Khalfan Ngassa, Hussein Masha, James Washokera, Hamza Mponda, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, Bea Simba, Kitwana Selemani, Nicco Bambaga, Juma Mhina, George Masatu na Paul Rwechungura.
Lakini leo Pamba imepotea sijui itarudi lini Ligi Kuu, maana imekuwa kama historia ambayo inasimuliwa kwa vijana wa siku hizi.
CDA na Kurugenzi (Dodoma)
Mkoa wa Dodoma ulikuwa na timu mbili zilizokuwa na upinzani mkubwa – Kurugenzi na CDA. Karibu kila timu iliyokuwa inatua mjini humo ilijua kazi ya klabu hizo.
Kurugenzi iliendelea kubaki daraja la kwanza kwa kipindi kirefu na
imepotea, lakini ilizalisha wachezaji wengi waliocheza katika timu za juu.
Kati ya wachezaji wake nyota ni Iddi Athumani ‘Pajero’, baba mzazi wa beki wa Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’, ambaye pia alichipukia mkoani hapo akicheza katika timu ya Polisi Dodoma.
CDA wao wanajipambanua kipindi hiki kutaka kurejea Ligi Kuu na kuja kuwapa furaha wakazi wa Mkoa wa Dodoma wanaoisikia Ligi hiyo kwenye bomba.
Dodoma sasa hakuna timu ya Ligi Kuu, lakini karibu kila kitu kuhusiana na soka imedorora. Dodoma umekuwa mji wa Bunge tu, dalili zinazoonesha wananchi wake kama hawana habari tena na mpira au wanaupenda lakini chama chao cha soka kimelala usingizi wa pono.
Tuwasubiri CDA labda watakuja kukonga nyoyo za watu hapo baadaye, maana wameonesha jitihada za makusudi kujipanga kutaka kurejea Ligi Kuu.
Milambo ya Tabora
Sifa ya Milambo inajulikana, hakuna kijana wa zamani asiyefahamu kazi ya Milambo. Tabora ni mkoa wa soka hasa.
Kumbuka enzi za Milambo au timu imara ya Mkoa ya Mashujaa wa
Unyanyembe. Tabora ni kati ya mikoa inayoongoza kwa vipaji vya soka, angalia wachezaji hawa wa enzi hizo na baadhi wanaoendelea kucheza.
Wachezaji ambao wametokea Tabora ni pamoja na Quresh Ufunguo, Ally Manyanya, Mikidadi Jumanne, Idd ‘Mnyamwezi’, Mrisho, Ally na Haruna Moshi ‘Boban’, Ahmed Mwinyimkuu, Said Mwamba ‘Kizota’, Athumani Shabani ‘Tippo’, Abubakari Kanyoro, Seif Juma, Ramadhani Hamis ‘Mvulana’, Mohamed Banka na wengine kibao.
Lakini sifa waliyokuwa wanajivunia kuwa na timu kubwa enzi hizo kama Milambo, ambapo Simba na Yanga wanajua shughuli zao.
Biashara ya Shinyanga
Timu hii ilianzishwa kwa kuitwa jina la RTC Shinyanga kabla ya kuitwa Biashara na baadaye Shinyanga Shooting.
Ilikuwa timu ya watu wa Shinyanga ikiwa na wachezaji kadhaa mahiri kama Michael Paul ‘Nylon’ ambaye baadaye alitikisa Simba, Paul John Masanja aliyetua Yanga na kuongoza ukuta mgumu na Mwinyimvua Komba ‘Masolwa’ aliyegoma mara kibao kujiunga na timu hizo kongwe akisisitiza anataka kubaki kwao.
Wapo wengine wengi kama Abdallah Magubika aliyetua Yanga baadaye, Alfred Kategile ‘Kate’ aliyekwenda Simba na Steven Nyenge ambaye pia aliwahi kuichezea Simba.
Lakini timu hiyo hadi leo imekufa na badala yake walau misimu hii
miwili Mkoa wa Shinyanga ina timu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, Mwadui FC na Stand United.
>>Itaendelea wiki ijayo…