Na Lookman Miraji, Jamhuri Mwdia, Dar es Salaam
Timu ya taifa ya mchezo kuogelea imefanikiwa kuibuka mshindi wa pili katika mashindano ya Afrika kanda ya 3 yaliyomalizika hapo jana jijini Bujumbura nchini Burundi.
Timu hiyo ya Tanzania imeshika nafasi hiyo mara baada ya kushinda alama 1642 nyuma ya timu ya taifa ya Uganda walioshika nafasi ya kwanza na mbele ya Kenya waliomaliza katika nafasi ya tatu.
Mbali na ushindi huo wa jumla, kamati ya mashindano hayo imewatambua baadhi ya waogeleaji kutoka timu ya Tanzania waliofanya vizuri katika vipengele tofauti tofauti vya umri wao.
Wafuatao ni waogeleaji wa kitanzania waliofanya vizuri katika mashindano hayo ya kanda ya tatu .
Nicolene Viljoen ameibuka kuwa mshindi wa kwanza kwa upande wanawake kati ya umri wa chini ya miaka 12.
Max Missokia ameibuka kuwa mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume walio chini ya miaka 12 huku, Fidel Kavishe akishika nafasi ya tatu katika kipengele hiko.
Crissa Dillip ameshinda nafasi ya kwanza kwa wanawake wenye umri kati ya 13 na 14, wakati
Julius Missokia akishinda nafasi ya pili kwa upande wa wanaume wenye kati ya miaka 13 na 14.
Filbertha Demello ameshinda nafasi ya pili kwa wanawake wenye umri wa miaka kati ya 15 na 16.
Wakati muogeleaji Romeo Mihaly Mwaipasi ameshinda nafasi ya pili katika kipengele cha waogeleaji wakiume walio chini ya umri wa miaka 17.
Timu hiyo taifa imewasili nchini hapo jana katika uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kupokelewa na viongozi kutoka baraza la michezo la taifa BMT wakiongozwa na Afisa michezo Charles Maguzu.