Mashabiki wa Liverpool wanaita ‘The Miracle of Istanbul” (muujiza wa Istanbul). Ni miaka 20 ilikuwa imepita tangu timu hiyo ilipotwaa Kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwaka 1985. Mhispania Rafael Benitez anawapa kombe hilo katika fainali dhidi ya AC Milan mwaka 2005.
Wanashinda kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka nyuma Milan wakiwa wanaongoza kwa magoli matatu hadi wakati wa mapumziko.
Mbinu za Benitez zinawarudisha Liverpool mchezoni ndani ya dakika zisizozidi 10 na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa ‘Mr Liverpool’ Steven Gerard kwa kichwa dakika ya 54, kisha Smicer akaandika goli la pili dakika ya 56 kabla fundi Xabi Alonso hajaisawazishia dakika ya 60.
Mechi inakwenda kwenye matuta baada ya dakika 120 kwisha kwa sare ya 3-3, Benitez anawapa ubingwa Liverpool baada ya kushinda kwa penalti 3 dhidi ya 2 za AC Milan kwenye fainali hiyo ilichozeshwa na Mhispania, Manuel Mejuto Gonzalez.
Benitez anageuka mfalme pale Liverpool, jina lake linaandikwa kwa kalamu ya almasi yenye wino wa dhahabu. Yeye anakuwa Liverpool na Liverpool inakuwa yeye. Lakini miaka mitano tu baada ya miujiza hiyo, Benitez anafukuzwa kazi Liverpool.
‘Papaa’ Mwinyi Zahera kutoka DRC alifanya Yanga isiyo na pesa kuwa tishio kwa Simba yenye kila kitu. Akashinda michezo 12 ya mwanzo katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Baadhi ya viongozi wakachukiwa kwa sababu yake. Akageuka lulu ndani ya Yanga. Msimu unaofuata walewale waliompenda wakamtupia makopo ya maji, wakamtukana, wakamzodoa na sasa jina lake limepotea kwenye midomo yao.
Hivi ndivyo kazi ya ukocha ilivyo. Maisha ya makocha ndani ya soka hayana tofauti na yale ya mende. Kushinda chooni, kulala sandukuni. Maisha ya makocha kwa mashabiki ni sawa na urafiki wa walevi. Siku pombe itakapopigwa marufuku duniani ndiyo siku watakayowajua marafiki wa kweli. Mashabiki wa soka wana maana yao kuhusu soka. Si Benitez peke yake tu na Zahera waliokumbwa na haya. Makocha wengi tu wenye majina makubwa duniani, waliozipa timu zao kila kitu lakini waliondoka kwenye klabu pasipo huruma hata ya kinafiki. Vicente Del Bosque katika miaka minne aliyoishi Real Madrid aliwapa mataji mawili ya la Liga, akawapa mataji mawili Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja la Super Cup. Yalipomkuta imebaki historia.
Alikuwepo Patrick Aussems pale Simba Sports Club. Akaipeleka Simba robo fainali ya Klabu Bingwa ya Afrika kwa mara ya kwanza. Chini yake Simba ikaogopwa na TP Mazembe, Al Ahly, AS Vita na klabu nyingine kubwa katika Bara la Afrika. Leo hata ‘followers’ wake Instagram wanazidi kupungua tangu aondoke Simba.
Hiyo ndiyo soka ilivyo tangu kipindi cha kina Franz Beckenbauer, Sir Matt Busby wa Manchester United miaka ya 1950 aliyefanya Manchester ibatizwe jina la ‘Busby babies’ kwa falsafa yake ya kuwaamini vijana wadogo.
Fabio Capelo aliishangaza Italia kwa kucheza mechi 58 mfululizo bila kufungwa, siku aliyofungwa katika mechi ya 59 maisha yake ndani ya Rossenari yakawa kama gari la mkaa. Safari moja shambani, safari ya pili gereji.
Jambo la ajabu kwa makocha ni kwamba kadiri anavyopata mafanikio ndivyo anavyojisogeza karibu na mdomo wa mamba. Mafanikio ya kocha wa mpira wa miguu ni sababu ya kupendwa pia ni sababu ya kuchukiwa. Ukitaka kufundisha mpira wa miguu duniani ujue kwanza jinsi ya kushinda mataji na jinsi ya kufukuzwa.
Soka si mchezo mgumu, bali mashabiki wake ndio wagumu. Katika mechi tatu za kwanza alizocheza kocha wa sasa wa Simba timu ilifunga magoli 12, mashabiki wakaimba nyimbo zote za mapambio kumsifia.
Alipoanza kukutana na chungu ya Ligi Kuu, mashabiki wale wale waliomsifia mwanzo ndio wanaotaka aondoke sasa. Luc wa Yanga alipokuja akapoteza mechi mbili dhidi ya Azam na Kagera. Sasa hivi timu inashinda na kuonyesha kandanda safi, lakini wanaomsifia ndio hao hao ambao walitaka atimuliwe baada ya mechi mbili tu!
Hakuna ujinga usio na ruhusa. Ujinga huu wa mashabiki wa soka kwa makocha umeruhusiwa na viongozi wa klabu. Bodi ya Klabu ya Real Madrid chini ya Rais Florentino Perez, Januari 4, 2016 inamtimua Benitez baada ya kelele za mashabiki kutokana na sare ya magoli 2-2 dhidi ya Valencia.
Maisha ya makocha yanatoa tafsiri sahihi kuhusu vipindi vya maisha ya binadamu. Kuna muda kwenye maisha kila kitu kinakubali. Hata ukikohoa utaambiwa sauti yako nzuri. Na kuna muda kwenye maisha kila kitu kinakataa. Huu ndio muda hata ukimsalimia mtu unaambiwa umemtukana.
Hii ndiyo soka, haina huruma kabisa na makocha. Hii ndiyo kandanda, ambayo mashabiki wasiojua mambo ya kiufundi wana nguvu kuliko makocha. Hawa ndio mashabiki wa kabumbu lililofanya mzee Wenger aachane na Arsenal kishingo upande. Wakasahau kuwa aliwapeleka fainali ya Klabu Bingwa ya Uefa mwaka 2005. Hawana shida na ‘unbeaten record’ yake ya msimu wa 2002/2003.
Mpaka sasa Ligi Kuu ya Tanzania Bara imeshuhudia makocha sita wakifungashiwa virago katika msimu wa 2019/2020 ambayo ndiyo kwanza imefika katikati. Hakuna kiongozi anayewajibika timu ikikosa matokeo hata kama sababu ya matokeo mabovu ni uongozi. Timu inayoboronga ni mali ya kocha, timu inayoshinda ni ya wote.
0629500908