Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetoa semina elekezi kwa wafanyabiashara, wajasirimali na wawekezaji  wa Mkoa wa Ruvuma ambayo imelenga kuwahamasisha wawekezaji kusajili  biashara zao sambamba na kufahamu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma na nchini kwa ujumla

Akizungumza kwenye ufunguzi wa semina hiyo,mgani rasmi katibu Tawala wa wilaya ya Songea Mtela Mwampamba ameishukuru TIC na  Serikali  kwa ujumla kwa juhudi za kuhakikisha inaandaa mazingira rafiki ya uwekezaji ndani ya Mkoa wa Ruvuma.

Amesema katika kuboresha miundombinu ya barabara mjini Songea kwa lengo la kuvutia wawekezaji,Manispaa ya Songea imepokea zaidi ya bilioni 22 za matengenezo ya barabara 22 kwa kiwango cha lami nzito.

Ameongeza kuwa pia serikali imetoa shilingi bilioni 19 za ujenzi wa masoko mawili ya kisasa  mjini Songea pamoja na kuboresha sekta ya viwanda ikiwa ni juhudi za Serikali kuboresha shughuli za uwekezaji nchini

“Tumeshaletewa pesa zaidi ya bilioni 22  kuhakikisha ndani ya manispaa barabara zote zinakuwa za lami, lakini kwa kutambua kwamba watu wa Ruvuma ni wawekezaji wakubwa, tayari tumeshapokea shilingi bilioni 19 ili tuweze kujenga masoko mawili ya kisasa  mjini Songea” Amebainisha

Naye Afisa Biashara Mkoa wa Ruvuma Joseph Martin Kabalo amezitaja fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Ruvuma ikiwemo  ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, fursa ya uuzaji wa bidhaa za viwandani, utalii, uvuvi na fursa ya usindikaji wa mazao mbalimbali hususani mahindi

 Felix John ni Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka TIC  amesema wapo Mkoani Ruvuma wakitekeleza kampeni ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani  ambapo wametembelea miradi  miwili ya wawekezaji wazawa wa ndani ya Mkoa wa Ruvuma.

Ameitaja miradi hiyo ni ya mwekezaji SUPERFEO aliyewekeza mradi wa kiwanda cha unga eneo la Namanditi mjini Songea na mradi wa uchimbaji wa makaa ya mawe unaofanywa na kampuni ya wazawa ya JITEGEMEE wilayani Mbinga.

Amesema TIC inatoa elimu endelevu ya   uwekezaji na kuhamasisha usajili wa miradi  ili wawekezaji waweze kunufaika na vivutio  vya kikodi na visivyo vya kikodi vinavyotolewa na Serikali.

Kwa upande wake Rosemary Ngonyani ambaye ni Mfanyabiashara Mkoani Ruvuma ameishukuru Serikali kupitia kituo cha uwekezaji kwa kutoa semina hiyo ambapo  amewahimiza wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma kukuza biashara zao na kuwekeza katika sekta mbalimbalimbali ili  kuepuka kuwategemea wageni kuwekeza katika sekta hizo;

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Ndicho chombo cha msingi cha Serikali cha kuratibu, kuhimiza, kukuza na kuwezesha uwekezaji nchini Tanzania.

Baadhi ya wajasiriamali na wawekezaji mkoani Ruvuma wakiwa kwenye mafunzo yaliyoendeshwa na TIC kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Huria mjini Songea 

Felix John Meneja Uhamasishaji na Uwekezaji wa Ndani kutoka TIC