Shughuli za uwekezaji duniani zimedorora kwa kiasi kikubwa miaka ya hivi karibuni na hii imetajwa kuwa sababu kubwa ya kupungua kwa mitaji binafsi kutoka nje (FDI), ambako kumejitokeza nchini tangu mwaka 2015, wataalamu wa sekta hii muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa sasa wamebainisha.

Wakizungumza na wahariri vya vombo vya habari kwenye semina maalumu mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) walisema kwamba pamoja na changamoto hiyo bado Tanzania itaendelea kuwa juu miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuvutia uwekezaji.

Sababu kubwa itakayoifanya Tanzania kuwa kinara wa uwekezaji ni uimara wa uchumi wake na kuendelea kukua vizuri kwa pato la taifa ambalo linategemewa kukua kwa wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Ukuaji huu utaifanya Tanzania kuipiku Kenya na kuwa na uchumi mkubwa katika Afrika Mashariki, ambalo ni eneo linalofanya vizuri kiuchumi barani Afrika. Vichocheo vikubwa vitakavyoifanya Tanzania kuongoza ni pamoja na uzalishaji wa viwanda unaotegemea rasilimali zake asilia, kuwa na vivutio vizuri vya kodi pamoja na maendeleo makubwa ya kanda za kiuchumi (special economic zones).

Takwimu za TIC zinaonyesha kuwa uwekezaji wa FDI nchini uliokuwa dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2013, ulipungua kwa asilimia 47.6 hadi dola bilioni 1.1 mwaka jana. 

Mwaka 2017, mitaji ya FDI nchini ilikuwa dola milioni 938 ukilinganisha na dola bilioni 1.4 mwaka 2016 na dola bilioni 1.6 na bilioni 1.4 mwaka 2015 na mwaka 2014 mtawalia.

Uwekezaji huu kwa Afrika nzima ulipungua kutoka dola bilioni 50.8 mwaka 2013 hadi dola 45.9 mwaka 2018, sawa na asilimia 9.6. Kwa dunia nzima, uwekezaji ulishuka kwa karibu asilimia tisa kutoka dola trilioni 1.4 hadi dola trilioni 1.2.

“Kushuka kwa kasi ya uwekezaji humu nchini kunatokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu na kimsingi ni kutokana na kupungua kwa FDI duniani kote na wala si mazingira mabaya ya kufanya biashara hapa kwetu kama inavyodaiwa na baadhi ya watu,” Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe, alifafanua.

Alisema changamoto za ndani zipo lakini mchango wake si mkubwa kama inavyodaiwa na ili nchi iweze kuwavutia wawekezaji na kuongeza mitaji kutoka nje, ushirikiano wa wadau mbalimbali ni muhimu sana. 

Kwa mujibu wake, bado hakuna uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa uwekezaji katika ujenzi wa uchumi wa kisasa na wenye tija na manufaa yake kwa watu walio wengi hasa wanasiasa na hata taasisi zinazohusika moja kwa moja kama idara za serikali na ofisi za umma.

Mwambe alisema eneo la uwekezaji ni sekta kuu mpya ya uchumi wa nchi ambayo inahitaji ushirikiano mkubwa kuiendeleza na kuifanya ichangie kikamilifu kwenye ukuaji wa pato la taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Pia alisema TIC inabidi kuungwa mkono na kufanya kazi kwa karibu na taasisi nyingine pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kuboresha mazingira ya biashara, kuzitangaza fursa za uwekezaji nchini na kuifanya Tanzania iendelee kuwa kivutio cha wawekezaji.

“Ili kujenga uchumi wa kisasa na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto na mahitaji ya kimaendeleo, uwekezaji uwe wa serikali au sekta binafsi hauepukiki. Tusipochangamka na kuwapata wawekezaji makini na mitaji ya kutosha, tamaa yetu ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda haitafanikiwa,” alifafanua.

Mwambe alisema mazingira ya uwekezaji na upatikanaji wa mitaji duniani yamekuwa magumu kutokana na sera za nchi nyingi kulinda masoko yao ya ndani, akitoa mfano wa Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump. Pia kuongezeka kwa misuguano ya kibiashara ikiongozwa na vita kati ya China na Marekani, kumekuwa na athari kubwa

hasa kwa nchi changa kama Tanzania.