DARE SALAAM
Na Aziza Nangwa
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesema miradi mipya 235 yenye thamani ya mabilioni ya fedha imesajiliwa katika kipindi cha mwaka 2020/21.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dk. Maduhu Kazi, anasema miradi hiyo inatarajia kuwekeza mtaji wa dola za Marekani bilioni 3.3 na kuzalisha ajira mpya 36,849.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia nane ya miradi iliyosajiliwa mwaka 2019/20.
“Katika kipindi cha mwaka 2020/21, TIC kwa kushirikiana na wadau mbalimbalii imetekeleza majukumu na kufanya uboreshaji uliosababisha kukua kwa uwekezaji nchini,” anasema Dk. Kazi.
Miongoni mwa uboreshaji huo ni wa Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre) ambapo taasisi zinazotoa huduma katika eneo hili zimeongezwa kufika 11.
Taasisi hizo ni Idara ya Kazi, Idara ya Uhamiaji, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Nyingine ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mamlaka ya Usimamizi wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
“Mafanikio mengine ni kuunganisha mifumo katika kituo hicho. Taasisi ina mfumo unaowawezesha wateja na wawekezaji kupata huduma kwa mtandao,” anasema Dk. Kazi.
Anasema kwa sasa TIC ina uwezo wa kutoa cheti cha vivutio ndani ya siku moja tu iwapo mwekezaji atakuwa amekamilisha nyaraka husika.
Uboreshaji mwingine uliofanyika ni wa utunzaji wa nyaraka ili kuhakikisha malengo ya TIC yanafikiwa kwa kutoa huduma ndani ya siku tatu tu.
“Kwa sasa TIC imejipanga kuhamasisha uwekezaji wa viwanda na kuboresha masuala ya upatikanaji wa ardhi katika kutekeleza Mpango wa III wa miaka mitano wa maendeleo, hasa katika uvutiaji wa uwekezaji,” anasema Dk. Kazi.
Kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2019/20, serikali imefuta au kupunguza ada na tozo zipatazo 54 zinazotozwa na wizara, idara na taasisi zinazojitegemea.
Kufuatia uboreshaji uliofanyika, miradi 99 iliyosajiliwa ipo Dar es Salaam, Pwani (34), Mwanza (15) na Dodoma (13).
Mingine ni Arusha (12), Shinyanga (11), Mara (9), Iringa na Tanga miradi minane kila mkoa, Morogoro (7), Geita (4), Lindi (3), Ruvuma (3), Kagera (2) na mikoa iliyobaki ina mradi mmoja mmoja.
Sekta iliyoongoza katika uwekezaji ni ya uzalishaji viwandani yenye miradi 138.