Utekelezaji wa sera ya taifa inayoelekeza halmashauri zote nchini kutenga rasmi maeneo maalumu ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji katika kila halmashauri nchini bado unasuasua na kusababisha kero kwa wawekezaji wa nje na ndani.
Sera hii ilikusudia kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wawekezaji, kwa mkakati wa kupunguza usumbufu na kuchelewa kupata hatimiliki kwa kutumia utaratibu wa kawaida.
Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) iliagiza halmashauri zote nchini kutenga, kupima na kumilikisha TIC maeneo maalumu ya ardhi kwa ajili ya wawekezaji wakati wowote inapohitajika.
Sera hii ni sehemu ya mkakati wa kutekeleza sera ya nchi ya kufanikisha uchumi wa kati wa viwanda.
Kusuasua kwa sera katika baadhi ya halmashauri kunadhihirisha kwa namna moja kukwazika kwa uwekezaji wa kiwanda cha sukari na mashamba ya miwa wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Mapema mwaka 2016 wananchi wa Tarafa ya Itiso, Kata na Kijiji cha Dabalo wilayani Chamwino katika Mkoa wa Dodoma walihamasishwa kulima zao la miwa baada ya kupatikana kwa mwekezaji wa kiwanda kidogo cha sukari kinachotarajiwa kujengwa katika kata hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Omary Kiguna, ameliambia gazeti hili kuwa baada ya mwekezaji kupatikana, wananchi walitoa zaidi ya ekari 30 bure kwa ajili ya kujenga kiwanda, wakati huo huo Bodi ya Sukari na Miwa ikawahamasisha wananchi kulima miwa sambamba na kuwapatia elimu pamoja na miche ya miwa.
Kiguna amesema zaidi ya wananchi mia moja wamelima zaidi ya ekari 1,800 za miwa licha ya kuwa baadhi ya wakulima wameshaanza kukata tamaa baada ya kuona hakuna kinachoendelea hadi sasa, kwani kiwanda hakijaanza hata hatua za awali za ujenzi.
“Wananchi wameanza kulima miwa tangu mwaka 2016, wamekwisha kulima na kuvuna mara kadhaa, kwa kuwa kiwanda bado hakijaanza, Bodi ya Miwa na Sukari imeamua kuingia gharama za kuinunua ili wakulima wasipate hasara, pia wasikate tamaa… lakini hili bado halitoshi, kwani hamu kubwa ya wananchi ni kiwanda, na hili limeshaanza kukatisha tamaa baadhi ya wakulima,” amesema Kiguna.
Taarifa za kuaminika kutoka sekta ya sukari zinakiri kuwa Bodi ya Sukari imeingia gharama ya kununua miwa hiyo kutoka kwa wakulima ili kuwasaidia wasipate hasara pamoja na kutowakatisha tamaa, na kusema kwa sasa mwekezaji amekwisha kukamilisha hatua zote na muda wowote ujenzi utaanza.
“Ni kweli tumekuwa tukiwalipa wakulima gharama zao za kulima, lakini pia tumekwisha kuwapatia elimu, ila niseme tu kuwa mchakato wa kupata kibali kwa mwekezaji umefikia hatua za mwishoni kabisa, na muda wowote ataanza ujenzi, hivyo wakulima kupitia chama chao cha ushirika wataendelea na mwekezaji wao,” kimesema chanzo hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Purandare Industries (Tanzania) LTD kutoka India, Satish Purandare, amekiri kukwazwa na ucheleweshaji wa kupata hatimiliki, lakini amedai kwa sasa anaamini mchakato upo katika hatua za mwisho.
Amesema anatarajia kuanza ujenzi Juni mwaka huu, na uzalishaji unatarajiwa kuanza Juni mwakani (2020) ambapo tayari alishapewa hati ya motisha (Certificate of incentive) tangu Januari mwaka 2017 na TIC ambayo hata hivyo kisheria haimpi uhalali wa kuwekeza bila kuwa na hati ya umiliki wa ardhi (Title Deed).
Kuhusu suala la wakulima wa miwa wanaoendelea kulima hadi sasa licha ya kuwa kiwanda bado hakijaanza uzalishaji, amesema ameingia makubaliano na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino pamoja na Bodi ya Sukari kwamba wakulima watalipwa na bodi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, amesema ucheleweshwaji wa hati miliki za ardhi kwa wawekezaji unasababishwa na halmashauri nyingi nchini kushindwa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji.
Mwambe amesema iwapo halmashauri zitatekeleza maagizo ya serikali ya kupima maeneo hayo, zoezi la kutoa hati kwa mwekezaji halitachukua zaidi ya miezi sita kutoka miaka miwili hadi mitatu kama ilivyo sasa.
“Hili suala la mwekezaji wa sukari kule Dabalo nalifahamu, tena juzi nimetoka kupitisha kibali chake cha umiliki wa ardhi, kwa hiyo suala hili limeshamalizika licha ya kuwa unaona limechukua muda mrefu lakini naweza kusema limechukua muda mfupi kutokana na mchakato unavyokuwa.
“Utaratibu wa kuhuisha ardhi unachukua muda mrefu, ndiyo maana tunaomba mabadiliko makubwa yafanyike, kuziomba halmashauri zipime maeneo yawe tayari watuletee sisi tuwe nayo, mpaka sasa ni halmashauri chache zimeshafanya hivyo, lakini nyingi bado, kwa kufanya hivyo itaturahisishia sana sisi, mwekezaji tutamwambia ardhi hii hapa chagua…” amesema Mwambe.
Amezishauri halmashauri za wilaya pamoja na watu binafsi wenye mashamba makubwa kupima maeneo ya mashamba na viwanda, kisha kupeleka katika benki ya ardhi ya kituo hicho ili kurahisisha kazi, ikiwa ni pamoja na kumpunguzia mwekezaji muda wa kusubiri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Athuman Masasi, amesema halmashauri hiyo imeshaanza zoezi la upimaji wa maeneo ya uwekezaji na hadi sasa wameshafikia kiwango cha asilimia 50 ya upimaji.
Amesema kabla ya kuanza zoezi la kutenga maeneo ya uwekezaji, ilichukua muda mrefu kwa mwekezaji hadi kupata hatimiliki ya ardhi, lakini kwa sasa maeneo yapo na kama itatokea mwekezaji anahitaji eneo, atapatiwa ndani ya muda mfupi tofauti na hapo awali.
Mwambe ameongeza kuwa licha ya kuwa maeneo mengi yamo mikononi mwa wananchi, lakini tayari wamekwisha kupata fedha kiasi cha Sh milioni 700 kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya mchakato wa upatikanaji wa ardhi za uwekezaji, ambapo ekari zaidi ya 300 zitapimwa.
Kwa mujibu wa mwekezaji, hatua ya kwanza ya ujenzi huo utagharimu dola za Marekani milioni 7.95, ambapo mwaka wa kwanza kiwanda kitazalisha tani 4,000 za sukari, kuanzia mwaka wa pili kitazalisha kati ya tani 6,000 na 8,000 huku wazawa zaidi ya 700 wanatarajiwa kupata ajira katika kiwanda hicho.