Profesa Anna Tibaijuka

*Akomesha viji-zawadi vya wawekezaji
*Wananchi kumiliki hisa kwenye ardhi
*Kigamboni kujengwa kwa trilioni 16

HATIMAYE Serikali imeridhia kufanya mabadiliko makubwa kwenye umiliki wa ardhi kwa kuwabana wawekezaji wanaojitwalia ardhi kubwa kwa kutoa viji-zawadi vidogo vidogo kwa halmashauri, vijiji na wananchi.
Kwa mabadiliko hayo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi sasa imeamua kuwa lazima wananchi wawe na hisa katika miradi yote ya wawekezaji.

Aidha, kinaanzishwa chombo maalumu cha kusimamia Hazina ya Ardhi.

Dhima kuu ya chombo hicho ni kusimamia utoaji ardhi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa misingi ya kuhakikisha wanaingia ubia wa kumiliki kwa pamoja hisa kati yao na wananchi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ameliambia Bunge kwamba kwenye mpango huo mpya, hisa zitatolewa kwa uwiano na thamani ya mtaji wa mwekezaji.

Profesa Tibaijuka alikuwa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake ya mwaka wa fedha wa 2012/2013, jana.

Alisema, “Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika zaidi na ardhi katika maeneo yao, na kuongeza usalama wa miradi ya wawekezaji. Kiwango cha chini cha hisa za Serikali katika ubia huo kitakuwa asilimia 25, na kati ya hizo mapendekezo ni kwamba angalau asilimia 5 zitagawiwa kwa Halmashauri yenye eneo hilo , asilimia 5 zitauzwa kwa bei ya soko kwa wananchi watakaotaka kushiriki katika miradi husika.”

Waziri huyo alitoa wito kwa wabunge kuunga mkono mpango huo mpya ambao umetajwa kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa.

“Naomba Bunge liunge mkono utaratibu mpya wa kutoa ardhi kwa wawekezaji kwa msingi wa kugawana hisa utakaofuta taratibu zinazotumiwa na Halmashauri na vijiji kwa sasa za kupewa gawio lisilozingatia msingi ya kichumi, kwa mfano wawekezaji kutoa zawadi ndogondogo kama visima vya maji, madarasa na kadhalika.

“Taratibu zitakapokamilika tutawasilisha muswada wa sheria ya kuanzisha rasmi chombo hicho,” alisema.

UJENZI MJI WA KIGAMBONI WAIVA
Kuhusu Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni, Profesa Tibaijuka, alitaja mambo yatakayofanywa katika mwaka huu wa fedha wa 2012/13.

Mambo hayo ni Wizara kusimamia uundwaji wa wakala, kuidhinisha mpango na kuanza utekelezaji, kufanya uthamini wa mali zilizomo katika maeneo ya miundombinu, huduma za jamii na eneo la makazi mbadala, kulipa fidia kwa mali zilizomo katika maeneo yaliyofanyiwa uthamini, kuandaa michoro ya kina, kupima na kuandaa ramani za ujenzi zilizomo katika eneo la makazi mbadala, kupima maeneo nje ya maeneo ya miundombinu kwa awamu na kuendelea na utekelezaji kwa awamu watatu.

Awamu ya kwanza ni kati ya 2012-2022, awamu ya pili ni kati ya 2022- 2027 na awamu ya tatu ni 2027-32.

Alisema gharama ya mradi inakisiwa kufikia Sh trilioni 11.6.

“Pamoja na kwamba asilimia 59 ya bajeti ya Wizara, takriban bilioni 60, zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kigamboni, kiasi hiki ni asilimia 10 tu ya pesa tunazohitajika mwaka huu. Kwa hiyo tutatumia mbinu za kisasa kutafuta pesa nyingine, takribani Sh bilioni 605 nje ya bajeti kutekeleza mradi huu bila kuchelewa zaidi.

“Mradi utahitaji kiasi hicho cha fedha kwa miaka 3 ya kwanza. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu wao na ushirikiano wanaotuonyesha na ninawahakikishia kuwa Serikali sasa imetenga bajeti ya kuhakikisha utekelezaji wa mpango huu unaanza na kushamiri.

“Nitasimamia mradi huu kwa karibu kwa kasi, ari na nguvu mpya. Ninataka kuanza na ziara za mafunzo kwa wawakilishi kutoka Kigamboni kutembelea miji mipya ili tuwe na uelewa wa pamoja juu ya kazi iliyo mbele yetu.  Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi watapewa maeneo ya kuanza kujenga makazi ambayo yatatumika kuwahamisha wananchi watakaopenda kubaki Kigamboni.

“Tunashauri ikiwezekana wote wachague kubaki maana hivi sasa kuna wananchi takribani 82,000 wakati tunajenga mji mpya wenye uwezo wa wakazi 400,000. Hakuna sababu ya wananchi kuhama eneo hili ila makazi yao yatapangwa upya na kuboreshwa. Serikali imeamua kuunda wakala mpya, Kigamboni Development Agency (KDA) kusimamia mradi huu wa kipekee katika historia ya Taifa letu.

“Wananchi ambao hawajakiuka maagizo ya mradi kwa kufanya maendelezo haramu, wasiwe na wasiwasi kuhusu fidia kwa sababu mradi utazingatia haki zao na ni endelevu. Fidia itatolewa kwa mujibu wa sheria, kwa tathmini ya kiujumla ambayo itakokotolewa kutokana na viwango vya soko na kuhuishwa ili iwe sahihi (land values under mass valuation),” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema mwaka huu wa fedha Serikali na wadau binafsi itaanza ujenzi wa Kituo cha Huduma Luguruni, Kwembe jijini Dar es Salaam .

WAVAMIZI WASITARAJIE FIDIA
Waziri Tibaijuka ametoa tahadhari kwa wavamizi wote wa maeneo yasiyoruhusiwa kwa kusema hawatalipwa fidia.

“Halmashauri zote nchini zinaagizwa zihakikishe kuwa zinapima viwanja na kuvigawa kwa wananchi ili kuepusha ujenzi holela.

“Wananchi wanaokaidi mipangomiji na kujenga kiholela, kuvamia maeneo ya wazi na kujenga katika maeneo yanayolindwa kisheria hususan fukwe na maeneo hatarishi, wasitarajie kupewa fidia wakati wa kuhamishwa. Tuko tayari kupokea maombi yenu kupewa viwanja au nyumba kuliko kupoteza akiba yenu kujenga visivyo,” alisema.

WALIOJENGA MSIMBAZI WAONDOKE
Profesa Tibaijuka amerejea wito wa Serikali wa kuwataka watu na taasisi zilizojenga ndani ya eneo la Bonde la Mto Msimbazi, kuondoka mara moja.

“Napenda kusisitiza tena kuwa eneo la Bonde la Mto Msimbazi ni eneo hatarishi kwa makazi ya binadamu, hivyo mamlaka za upangaji zichukue hatua za haraka kuondoa makazi na maendelezo yote yaliyofanyika humo kwani hayana mustakabali. Ni dhahiri kwamba maafa ya mara kwa mara katika eneo hilo hayaepukiki hasa ukizingatia mabadiliko ya tabianchi.

“Vilevile, naagiza Halmashauri zote kuainisha maeneo yote hatarishi, hususan mabonde na milimani na kuyawasilisha kwangu kwa ajili ya kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali. Natoa wito kwa wadau wote, kutoa ushirikiano unaostahili ili kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa manufaa ya wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine,” alisema.

WALIOHODHI ARDHI KUNYANG’ANYWA
Waziri Tibaijuka alisema Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 inatambua kuwa ardhi yote ni mali ya umma hivyo mfumo wa kumiliki ardhi ni ule wa haki ya kutumia na siyo kuhodhi.

Kwa maana hiyo, alisema kila anayemilikishwa ardhi ana wajibu wa kuiendeleza kwa matumizi yaliyopangwa na asipofanya hivyo hatua za kufuta milki hizo zitachukuliwa na kurudisha mikononi mwa Rais.

Aidha, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji Ardhi, Na. 47 ya mwaka 1967 (Sura ya 118) pale ambako ardhi itahitajika kwa manufaa ya umma itatwaliwa kwa mujibu wa sheria hii.

“Utaratibuwa utwaaji na ubatilishaji unaanzia ngazi ya Halmashauri hadi ngazi ya Taifa. Katika kutekeleza majukumu haya kwa mwaka 2011/12, ilani za ubatilisho zilizotumwa ni 792 na jumla ya milki 72 zilibatilishwa na kutwaliwa na milki 1,512 zilihamishwa.

Kwa mwaka 2012/13 Wizara yangu itaendelea kutwaa ardhi na kubatilisha milki kwa mujibu wa sheria na inatarajia kushughulikia maombi 1,700 ya uhamisho wa milki.

“Ili kuhakikisha kuwa ardhi inatumika kwa ufanisi natoa agizo kwa Halmashauri zote nchini kuwasilisha wizarani taarifa za viwanja na mashamba yaliyotelekezwa au kutumika kinyume na masharti ya milki ili taratibu za kubatilisha milki ziweze kuchukuliwa,” alisema.

HOTUBA KAMILI YA WAZIRI TIBAIJUKA SOMA UK . 7