Na DottoKwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
BENKI ya Maendeleo(TIB)imesema imezalisha zaidi ya ajira mpya 12,547 kutokana na Benki kufadhili miradi ya muda wa kati na mrefu nchini inayotokana na uwekezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maeneo ya kipaumbele ya Serikali pamoja na malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Lilian Mbassy ameeleza hayo leo March 20,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema uwekezaji huo ni wa miradi ya muda wa miaka 5-15 katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Amesema uwekezaji huo umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 630.3 katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024 mbapo kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 408.3 zipo kwenye mizania ya Benki,huku mifuko tisa inayosimamiwa na Benki ikichangia uwekezaji wa Shilingi bilioni 222.
“Uwekezaji huo umegusa maeneo ya kipaumbele ya Serikali pamoja na malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambapo bil.162.7 zimewekezwa kuongeza usalama wa chakula na kupunguza njaa,
Aidha shilingi bilioni 4.3 zimewekezwa
kuboresha elimu kupitia miradi ya taasisi za elimu na Shilingi 22.4 bilioni zimewekezwa katika upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kupitia miradi ya mamlaka za maji, “amesema.

Mkurugenzi huyo ameutaja Uwekezaji mwengine wa Shilingi 11.5 bilioni kuwa umewekezwa katika nishati safi na nafuu kupitia mradi wa upanuzi wa nishati ya umeme vijijini (Tanzania Rural Electrification Expansion Programme-TREEP).
“TIB kama benki ya maendeleo ni taasisi ya kisera ambayo ina jukumu la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa hususani kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo mwaka 2025,
vipaumbele vyetu vimejikita katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo,pamoja na kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita, “amesema
