Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamelitaka Jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio la utekwaji na mauaji ya kikatili ya Mtoto Asimwe Novati.

Aidha wametoa wito Kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutumia kipindi hiki cha Bunge la bajeti kujadili na kuweka vifungu maalum ili kuimarisha mifumo ya ulinzi wa kwa watu wenye ualbino.

Mei 30, 2024 kuripotiwa tukio la kutekwa kwa mtoto wa miaka miwili (2) mwenye ualbino ililiofanywa na watu wasiyojulikana katika Kijiji cha Bulamula, Kitongoji cha Mbale, Kata na Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera.

Iliripotiwa kuwa watu hao walimvamia kwa kumkaba mama wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Kebyera Richard, na kisha kumchukua na kukimbia na mtoto huyo kusikojulikana. Takribani siku kumi na nane (18), na Juni 17, mwaka huu iliripotiwa kupatikana kwa mwili wa mtoto huyo ukiwa umekatwa viungo vyake ikiwemo mikono, ulimi na macho.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 19, 2024 Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Fulgence Massawe amesema wanalaani vikali tukio hilo kwani linaweka taswira mbaya kwa nchi na kuonyesha kuwa hakuna usalama kwa watu wake hususani watu wenye ualbino.

Amesema ni tukio la kinyama, linalotweza utu wa mwanadamu na kurudisha upya taswira mbaya iliyotokea miaka michache dhidi ya ukatili wa watu wenye ualbino.

“Tukio limeendeleza kumbukumbu za matendo ya kikatili, tangu kunusurika kifo kwa mtoto mwenye ualbino aitwaye Kazungu Julius mwenye umri wa miaka kumi (10) mkazi wa Katoro mkoani Geita baada ya kuvamiwa na watu wasiyojulikana na kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea kuvuja damu nyingi.

“Ni wazi kuwa mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino yamerudi kwa kasi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi hasa kwa watoto, itakumbukwa mwaka 2015 mkoani Rukwa kulitokea tukio la kushambuliwa kwa mtoto wa kiume aitwaye Baraka Cosmas mwenye umri wa miaka sita (6) akiwa amelala na mama yake mzazi ambapo watu wasiyojulikana walivamia nyumbani kwao na kumkata kiganja,” amesema.

Amefafanua kuwa, tukio hilo ni ukiukwaji wa wazi wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inabainisha ulinzi wa haki ya kuishi, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu, 2006, Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu pamoja na sheria za nchi ikiwemo Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura Namba 16 (Marejeo ya 2019).

” THRDC na LHRC inalaani vikali vitendo hivi vya kikatili, kinyama na kihuni dhidi ya ndugu zetu wenye ualbino. Kwa kipekee tunatoa pole na tunasimama na familia ya marehemu Asimwe Novati katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Hakuna mtoto anayestahili kufanyiwa vitendo vya kikatili namna hii kwa sababu ya hali au mwonekano wake,” amesema.

Naye Meneja WA THRDC, Remy Lema amesema hawajaridhishwa na mwitikio wa mamlaka husika ikiwemo kutoa taarifa kwa umma kujulisha jitihada zilizochukuliwa punde baada ya taarifa ya kupotea kwa mtoto huyo, pia hakukuwa na taarifa yoyote kwa umma juu ya kuwatafuta watu waliofanya tukio hilo.

“Jambo hili linaongeza hofu kwa jamii ya watu wenye ualbino kuhusu usalama wao katika nchi yenye amani na sifa ya kulinda Haki za Binadamu.

“Tukio hili la kinyama na kikatili dhidi ya mtoto huyu mwenye ualbino linapaswa kuikumbusha serikali na mamlaka zote husika kuhusu uhitaji mkubwa wa juhudi za pamoja za kukabiliana na unyanyasaji na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino katika jamii zetu,” amesema.

Aidha ametoa wito kwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) kuweka mikakati madhubuti ya kuwatambua na kusimamia ustawi watu wote wenye ualbino katika maeneo yote ya nchi.

“Tunatoa wito pia Kwa jamii kuripoti watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ili vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za kipelelezi na kuachana na imani potofu juu ya matumizi ya viungo vya watu wenye ualbino kwa kuhusisha na utajiri au kujipatia mamlaka katika ngazi mbalimbali.

“Tunawahimiza wanajamii wote kusimama pamoja kuibua na kutoa taarifa juu ya watu wote wanaofanya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa sababu ya imani za kishirikina,” amesema Lema.

Please follow and like us:
Pin Share