Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imelaani kitendo cha video inayosambaa katika mitandao ya kijamii inayoonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti na ambapo imesema kitendo hicho sio cha kiungwana na hakikubariki popote.
Hayo yameelezwa leo Agosti 7,2024 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora JajiMstaafu Mathew Mwaimu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye banda la tume hiyo lililopo katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni.
“Sisi kama Tume tunaona binti huyo alifanyiwa unyanyasaji na amenyimwa haki yake za ubinadamu wake, utu wake amedharirishwa katika utu wake na vilevile ni kitendo ambacho hakikubariki kwasababu kinaonekana kiliandaliwa nani bahati mbaya sana kwamba inaonekana kiliandaliwa na mtu ambaye alikuwa anafahamu kinachoendelea”, amesema.
Aidha ameongeza kuwa wanaamini ofisi ya mashtaka itaweza kuwafungulia watu hao mashtaka ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na wakikutwa na hatia waweze kupatiwa adhabu kari.
“Tunaamini kwamba vitendo hivi havifai ni jambo baya sana kwamba katika nchi kama hii kwa miaka mingi tumeamini kwamba watu wanazidi kuwa wastaarabu lakink wanafanya vitendo ambavyo havifai”,ameongeza.
Ikumbukwe kuwa Agosti 4, mwaka huu zilisambaa video katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo, huku wakimtuhumu kwa kile kilichosikika katika video hiyo kuwa ametembea na mume wa mtu,
Na binti huyo alisikika akieleza anakotokea na kumwomba msamaha mtu aliyetambulishwa kwa jina la Afande.