TGNP Mtandao imeanzisha kijiwe maalum cha hedhi kwa wanawake ili kuwawezesha watoto wa kike shuleni kujadili juu ya mwenendo wa hedhi salama.

TGNP Mtandao imefikia uamuzi huo wa kuanzisha kijiwe cha hedhi baada ya kubaini uwepo wa watoto wengi wa kike kushindwa kupata taarifa sahihi juu ya afya ya uzazi na hedhi salama, jambo linalochangiwa na baadhi ya mila na desturi potofu.

Akizungumza jana katika kijiwe kilicho wakutanisha wanafunzi wa shule za mbalimbali za Dar es Salaam, Meneja wa Idara ya Ujenzi wa nguvu ya Pamoja wa TGNP Mtandao, Grace Kisetu alisema wasichana wanatakiwa kuwa huru kujadili wanapojadili masuala yanayohusu afya zao.

“Unajua watoto wetu wakati mwingine wanakutana na vitu ambavyo kwa sababu ya mila na desturi wanashindwa kusema wazi, sasa tumeamua kuanzisha kijiwe kukaa nao na kuwasaidia…wasione haya kulizungumzia suala hili (hedhi),” alisisitiza Bi. Kisetu.

Aidha, akifafanua zaidi alisema mjadala kuhusu hedhi salama utaiamsha jamii ambayo imekua ikifikiri kuwa jambo hili ni siri kuzungumziwa wakati wapo wasichana ambao wamekuwa wakiumia kwa kutowekewa mazingira salama pindi wanapokuwa katika hali hiyo.

Pamoja na hayo takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET), zinabainisha kuwa asilimia 82 ya wasichana nchini Tanzania hawana taarifa sahihi kuhusiana na mabadiliko ya miili yao na namna sahihi ya kukabiliana na changamoto kipindi cha hedhi.

Hali ya kutokuwa na taarifa sahihi imechangia baadhi ya mabinti hao kuathiriwa kimasomo kwa kile kushindwa kuhudhuria vipindi shuleni wanapokuwa katika hedhi zao.

Naye Mwalimu Ester Chaduo wa Shule ya Msingi Makumbusho, akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema wameanzisha utaratibu wa kuwasaidia wasichana kupata elimu kuhusu afya zao kwa kukaribisha wadau kulizungumzia jambo hilo pamoja na kugawa bure taulo za kike kwa wanafunzi wasioweza kuzipata kutokana uduni wa kipato katika familia zao.