Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

WAKALA wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Mashariki umewataka wananchi kuchangamkia fursa ya ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali kwa wingi ili kuongeza kipato na kufikia masoko ya kimataifa.

Ofisa Nyuki wa TFS, Happiness Kivuyo, akizungumza kuhusu umuhimu na faida za ufugaji wa nyuki pamoja na utalii wa nyuki, alibainisha kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu kilimo cha nyuki na upatikanaji wa masoko.

“Wafugaji wanapaswa kuhakikisha ubora wa asali wanayozalisha ili kupata kibali cha kuuza kwenye masoko ya kimataifa,” alisema Kivuyo.

Aliongeza kuwa mahitaji ya asali yameongezeka, hususan katika nchi za Kiarabu, na TFS inajitahidi kutoa elimu pamoja na vifaa kwa wafugaji wadogo ili kusaidia kuongeza uzalishaji na kuuza bidhaa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Kivuyo, sekta mpya ya Utalii wa Nyuki (Api-tourism) inalenga kuvutia wageni kushiriki shughuli kama kudungwa na nyuki kwa tiba na kununua mazao ya nyuki yaliyoboreshwa, kama asali, chavua, karanga za asali, na maziwa ya nyuki, ambayo hutumika kama dawa na virutubisho vya mwili.

Naye Veronica Kombe, Mhifadhi wa Mambo Kale wa TFS Bagamoyo, alisema utalii wa nyuki pia unahusisha kutembelea mizinga ya nyuki, kujifunza kuhusu faida zake, na kununua bidhaa za nyuki.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa TFS, Shaban Kiula, alisema taasisi hiyo inaendeleza juhudi za kukuza utalii wa nyuki kama sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya kuongeza sekta ya utalii nchini.

“Nyuki si kwa ajili ya uzalishaji wa asali pekee, bali pia kwa tiba. Kwa mfano, kulingana na uzito wako, nyuki wanaweza kukuuma na kutoa tiba maalum,” alifafanua Kiula.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanal Joseph Kolombo, alisisitiza umuhimu wa TFS kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa taifa kwa ujumla.