Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) bado una watendaji dhaifu.

Wanatakiwa kusimamia sheria ili watumiaji wa mazao ya misitu wazingatie yaliyomo kwenye Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 ambayo pia inatambulika kama Sheria ya Misitu Sura Namba 323 (RE: 2002), Kanuni na Miongozo inayoelekeza taratibu za uvunaji, usafirishaji na jinsi ya kufanya biashara ya mazao ya misitu.

Sheria na Kanuni inaelekeza yafuatayo:

Mosi, kila mvunaji wa mazao ya misitu lazima awe na leseni halali ya uvunaji wa mazao ya misitu iliyotolewa na mamlaka husika. Kila gunia la mkaa lililobebwa na chombo chochote cha usafiri ni lazima liwe limekatiwa risiti halali ya malipo ya serikali.

Pili, kila msafirishaji wa mazao ya misitu lazima awe na kibali (Transit Pass – TP) cha kumruhusu kusafirisha mazao ya misitu ikionesha mahali mazao hayo yalipotoka na yanapokwenda ikiambatishwa na leseni ya uvunaji.

Tatu, kila mfanyabiashara lazima awe amesajiliwa na TFS kuwa ni mfanyabiashara halali wa mazao ya misitu.

Nne, usafirishaji wa mazao ya misitu ni kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni.l

Tano, ni marufuku kusafiriksha mkaa kwa kutumia pikipiki zinazotumia matairi mawili.

Sita, biashara ya mkaa lazima ifanyike katika maeneo maalum yaliyoanishwa katika kila wilaya.

Saba, ni marufuku kwa wafanyabiasha ya mkaa kufanya biashara hiyo kandokando ya barabara.

Nane, kwa wanunuzi wote wa mkaa kwa ajili ya matumizi ya kaya ni lazima wawe na risiti halali ya Serikali inayoonesha malipo yaliyofanyika kwa idadi ya magunia ya mkaa aliyonunua.

Jambo la kusitikisha ni kuona TFS bado imelala usingizi huku mamia ya malori, yakibeba mkaa tena ndani ya makontena na magari yaliyofunikwa (jambo ambalo ni kinyume cha sheria) bila kuchukuliwa hatua.

TFS bado wapo kwenye usingizi wa pono. Wiki iliyopita Wakala wa Vipimo Kanda ya Kinondoni walianza kukamata malori yaliyopakia mazao rumbesa pale kwa Musuguri jijini Dar es Salaam.

Kwa kuwa malori yote yanapakia mkaa bila vibali, na kwa kuwa biashara hii inafanywa pale kwa Musuguri, TFS wanasubiri nini kuwakamata watu hawa? Je, Waziri wa Maliasili na Utalii anashindwa nini kuzuia uharibifu huu unaoangamiza misitu nchini?

Viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakitumbuliwa watamlaumu Rais Magufuli? Tunashauri ukaguzi uanze sasa Kwa Musuguri ili kuyakamata malori haya. Hatua hiyo itachochea matumizi ya gesi na hivyo kuokoa misitu. TFS wasisubiri kutumbuliwa.