Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imetoa wito kwa Wakulima kujisajili katika mfumo wao pamoja na kutoa taarifa zilizo sahihi ili kuweza kupata mbolea ya ruzuku.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa uzalishaji wa ndani na ununuzi wa mbolea kwa pamoja, Louis Kasera wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane-Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema hadi Sasa wakulima Milioni 4 wamesajiliwa huku lengo likiwa kusajili Wakulima milioni 7 Nchi nzima.

“Wale ambao wamesajiliwa kipindi cha nyuma sasa tunaenda kuwachukua alama za vidole, picha zao lengo ni kujua mkulima yupo wapi, ni nani ili serikali ijue itampata wapi,’ amesema.

Amefafanua kuwa, kwasasa kuna tani za mbolea zaidi ya 300,000 ya kupandia na ya kukuzia na kwamba hali ya mbolea ni ya kujitosheleza ambapo lengo kwa mwaka huu ni wakulima kuchukua tani 1,000,000.

“Kama mnavyojua tunakaribia kuanza msimu mpya, na tuna asilimia 30 ya mbolea ndani ya nchi na kwamba kuna meli zipo njiani ambapo tunatarajia msimu utakapoanza tutakuwa na asilimia 50 na itakapofika Disemba tutakuwa tumeingiza mbolea zote zinazotoka nje,” amesema.

Ameongeza kuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha mkulima anapata mbolea bora huku akisema kwa sasa wamefungua Maabara ili kuhakikisha mbolea hizo zinazoingia zina viwango vinavyotakiwa.

Amebainisha kuwa, kwa miaka miwili iliyopita wamekuwa wakitoa mbolea ya ruzuku huku akimshukuru Rais Dk. Samia suluhu Hassan baada ya kuona mbolea hiyo inapanda bei kutokana na vita ya Ukraine na COVID-19 aliamua kuweka Ruzuku mwaka 2022/ 2023.

“Lakini amendelea kutoa ruzuku kutoa ruzuku hii na tuendelee kuitoa hadi mwaka 2025/2026, hii ni kwa ajili ya kumsaidia mkulima apate mbolea kwa bei rahisi imfikie pale alipo ili waweze kuongeza tija katika kilimo biashara na aweze kupata mazao mengi ya chakula na aweze kuuza,” amesema.