Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

AFISA Utafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Francis Millinga ametoa wito kwa jamii kuacha dhana potofu kwamba Virutubishi vina madhara.

Ameyasema hayo kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ambayo yanafanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni-Nanenane jijini Dodoma.

Amesema kuwa Taasisi hiyo wanaprogramu uongezaji Virutubishi kwenye chakula ambapo kwa kushirikiana na wadau wengine Tanzania wakiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI).

“Watanzania wamekuwa na dhana potofu kuwa Virutubishi vina madhara. Dhana hii sio ya kweli kwani vimethibitishwa na TBS na kila kinachoingia kinachukuliwa na kupimwa.

“Kwahiyo niwaombe waache dhana hii potofu kwani inawakwamisha jitihada za serikali katika kuboresha masuala mazima ya lishe kwa jamii,” amesisisitiza.

Aidha amesema kuwa muda si mrefu wasagishaji wote wa lishe nchini watatakiwa kuongeza virutubishi kwenye vyakula ambapo tayari kanuni zimeshaandaliwa.

Ametaja Virutubishi hivyo ni vitamini B12 ‘Folic acid’ ambavyo vitawekwa kwenye unga wa ngano na mahindi wanaweka madini chuma na zinki ‘zinc’ ambapo mafuta ya kula wanaweka vitamini A na chumvi huongezwa madini joto.

Ameongeza kuwa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na TBS wanahakikisha kila mwenye mashine kuweka na kinyunyuzi cha virutubishi.

“Kanuni imeshapitishwa wasagishaji wote na wengine hawa wadogo kanuni imeshapita itaanza kusimamiwa hivyo waongeze virutubishi kwenye chakula lengo ni kuondokana na vifo vya akina mama wenye umri wa uzazi miaka 15 hadi 49 ambao mara nyingi huwa wanapoteza maisha kwa kukosa damu,” amesema.

Amebainisha kuwa Kiwanda kimeshafunguliwa Mikocheni jijini Dar es Salaam cha kutengeneza virutubishi hivyo.