ALIPOCHAGULIWA kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF), beki wa zamani wa kimataifa wa Yanga na Pan African, Leodgar Chillah Tenga alitarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya soka hapa nchini.

Alitegemewa kuanzisha programu mbalimbali zinazolenga kuiweka Tanzania katika ramani ya juu ya soka kuanzia ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kusini mwa Jangwa la Sahara na hata Afrika, matumaini ambayo idadi kubwa ya wadau walikuwa nayo.

 

Alidhaniwa kuwa angeiongoza TFF yenye nidhamu katika utendaji wake, sikivu kwa wadau wake, inayojali na kuheshimu ratiba za kimataifa za kandanda hasa kwa kuzingatia kuwa ni mwanachama wa Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA), Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF) na hata vinginevyo.

 

Lakini tangu Tenga achukue uongozi huo wa juu kabisa wa TFF, mashabiki wa soka nchini wamebaki wakijiuliza endapo nchi yetu inapiga hatua kwa maendeleo ya mchezo huo au iko palepale, vilevile ama inarudi nyuma.

 

Bado ugonjwa mkubwa wa kuvuruga kila jambo zikiwemo ratiba za Ligi Kuu, usajili  wa wachezaji na kadhalika unaendelea kuitafuna soka yetu. Hakuna mabadiliko yoyote ya kimsingi yanayoonekana kufanyika nje na ndani ya dimba.

 

Pamoja na kusaidiwa katika utendaji wa kila siku na waandishi mahiri wa habari za michezo ambao ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Ossiah na Afisa Habari wake, Boniface Wambura, mambo bado yanaendeshwa kwa mtindo wa zimamoto. Tayari zoezi la usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom na ile ya Daraja la Kwanza Tanzania Bara umeshavurugwa.

 

Kwanza ilikuwa inafahamika kwamba mwisho wa zoezi hilo ilikuwa Agosti 10, mwaka huu, lakini ilipokuwa inafika, ghafla Angetile akaibuka na kutangaza kuwa lingeendelea kwa siku tano zaidi na hivyo kuhitimishwa rasmi Jumatano ya Agosti 15.

 

Kila tarehe zinazowekwa na kutangazwa kwa waandishi wa habari kulikuwa hakuna sababu hasa za msingi zinazotolewa, badala yake ilikuwa ikidaiwa kuwa inatokana na mkanganyiko wa tarehe kwa vilabu. Hata mwisho huo wa pili ulipofika, Katibu Mkuu wa TFF aliibuka tena na kutangaza vingine. Alisema kuwa usajili wa wachezaji wa ndani peke yake ndio umemalizika Jumatano iliyopita, lakini ule wa wachezaji wa kulipwa kutoka nje ya nchi utaendelea hadi Septemba 15.

 

Nafasi hiyo kwa wachezaji wa kulipwa inahusu fomu ya uhamisho kutoka timu aliyoichezea msimu wa mwaka 2011/2012 kwenda klabu anayohamia, na pili ni fomu inayotoka Chama cha Soka cha nchi anayotoka kuja TFF, maarufu kama ITC.

 

Timu ambazo zitacheza Ligi Kuu ya VodaCom Tanzania Bara katika msimu ujao mbali na mabingwa watetezi au Simba ni pamoja na washindi wa pili, Azam FC, Yanga na African Lyon (zote za Dar es Salaam), Coastal Union (Tanga), JKT Oljoro (Arusha), JKT Ruvu na Ruvu Shooting (za Kibaha, Pwani), Mtibwa Sugar (Morogoro), Kagera Sugar ya Kagera na Toto African ya Mwanza.

 

Nyingine ambazo pia zitacheza Ligi Kuu msimu huu baada ya kupanda kutoka Ligi Daraja la Kwanza ni Polisi ya Morogoro, JKT Mgambo (Tanga) na Prison ya Mbeya zilizochukua nafasi za Villa Squad (Dar es Salaam), Moro United (Dar es Salaam) na Polisi ya Dodoma.

 

Hatua ya TFF ya kusogeza mbele tarehe ya mwisho ya usajili kwa wachezaji wa kulipwa, inaaminiwa na wadau wengi wa soka nchini kuwa inalenga kuzibeba Simba na Yanga ili zikamilishe zoezi hilo.

 

Zote mbili ziliingia katika malumbano makali mwishoni mwa usajili huo kwa kugombea baadhi ya wachezaji na kuziba mapengo kadhaa. Mbali na kumgombea beki wa kati kutoka APR ya Rwanda, Mbuyu Twite ambaye kwanza aliingia mkataba wa kuja kucheza kandanda akiwa Msimbazi, kisha akasaini kwenda katika Mitaa ya Twiga na Jangwani, timu hizo pia zilichelewa kuziba mapengo yake.

 

Simba iliwatimua katika dakika za mwisho wachezaji Lino Masombo na Nkanu Mbiyavanga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Yanga ikawatema kwa namna ileile washambuliaji Davis Mwape wa Zambia na Kenneth Asamoah wa Ghana.

 

Wote hao nafasi zao zilichukuliwa na Twite (ambaye Simba ilisalimu amri kwake) na mshambuliaji Didier Kavumbagu waliosaini Yanga, na Simba ikasajili beki aliyetoka AFC Leopards ya Kenya, Patrick Ochieng na mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Daniel Akuffo.

 

Kusajiliwa kwao katika dakika za mwisho ndiko kunaaminiwa na mashabiki wengi kwamba, TFF imelazimika kusogeza mbele zoezi la usajili wa wachezaji wa kulipwa hadi Septemba 15. Hii ni kwa vile sehemu zote duniani hakuna kunakokuwa na ratiba mbili za usajili kati ya wanasoka wa ndani na kutoka nje ya nchi ila msimu huo unakwenda kwa wakati mmoja.

 

Aidha, hata Tanzania hatua hiyo ndiyo kwanza imeanza mwaka huu, halafu imeibuliwa ghafla na TFF baada ya Simba na Yanga kuchelewa kufanya hivyo. Kama zingemaliza usajili huo kwa muda wa kawaida, bila shaka hakuna hata siku moja ambayo ingeongezwa. Hiyo inaendeleza udhaifu mkubwa wa uongozi wa kandanda ndani ya shirikisho hilo chini ya Leodgar Tenga na Angetile Ossiah.

 

Tumekuwa tukishuhudia mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba za michezo ya Ligi Kuu na kusababisha baadhi ya timu kuwa mbele kwa mechi zilizocheza huku nyingine zikiwa nyuma, baadhi zikitakiwa kucheza mara mbili au hata tatu ndipo zikamilishe viporo vyake, hali inayozaa malalamiko ya kupanga matokeo au kuwahonga waamuzi hasa wa kati.

 

Haieleweki kwa nini tuendelee na uendeshaji huu wa zimamoto kwa soka la Tanzania uliogeuka sehemu ya kawaida. Kila msimu sasa umekuwa ukikumbwa na matatizo mbalimbali, yale ambayo yanachangia kwa namna moja ama nyingine kupunguza ushindani wa ndani ya dimba kati ya timu shiriki za ligi hiyo.

 

Kama ilivyokuwa msimu uliopita, mechi mbili zilizoihusu Azam FC ziliharibika baada ya kuonekana kuwepo mashaka dhidi ya waamuzi ambapo walipigwa. Kwanza ilikuwa mechi kati ya timu hiyo na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikawa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma dhidi ya timu ya Polisi ya huko.

 

Simaanishi moja kwa moja kwamba kusogezwa mbele kwa tarehe ya mwisho ya usajili wa wachezaji wa kulipwa kumeharibu ligi nzima, lakini madudu hayo ya TFF tayari yameanza kuiharibu hatua kwa hatua na huenda ikaendelea kuwa na matatizo zaidi kama ilivyokuwa msimu uliopita. Imeanza kuonyesha waziwazi upendeleo na ubaguzi miongoni mwa timu 14 za Ligi Kuu.

 

Licha ya michuano hiyo kupangwa kutimua vumbi kuanzia Oktoba Mosi, yapo madai kuwa hata udhamini wake hadi sasa haueleweki. Inasemekana TFF inafanya mazungumzo ya siri na kampuni moja ya bia nchini ili iwe ndiye mdhamini mpya, lakini hayo yanaendelea huku ikiwa bado haijavunja mkataba wake na VodaCom Tanzania.