Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeelezwa kuwa ni taasisi bora barani Afrika inayoheshimika na kuaminika na Shirika la Afya Duniani (WHO), kutokana na utendaji wake uliokidhi viwango vya ubora.
Hayo yameelezwa wiki iliyopita na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwa mikoa ya Kanda ya Kati kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura Na. 219 mjini Dodoma.


Dk. Rashid anasema TFDA imekuwa ni taasisi inayoongoza kwa ubora miongoni mwa taasisi zote nchini na barani Afrika, huku ikiombwa kutoa mafunzo kwa maofisa wa nchi mbalimbali.
Anasema kutokana na kuaminika kwake, TFDA iliteuliwa na WHO kufanya ukaguzi katika viwanda nchini India na kuvifunga baadhi vilivyokosa ubora hadi vilipokamilisha vigezo vilivyokuwa vinatakiwa.
“Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuboresha utoaji huduma, mwaka 1990 ilianzisha programu ya kuboresha utoaji huduma katika sekta ya umma ili kufikia matarajio ya jamii ikiwa ni pamoja na kuanzishwa wakala mbalimbali ikiwamo TFDA,” anasema waziri wa Afya.
Anasema tangu kuanzishwa kwake, TFDA imekuwa na wajibu mkubwa wa kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, na kwamba bidhaa hizo ni muhimu na zenye madhara makubwa ya kiafya, na kama hazitadhibitiwa ipasavyo zinaweza kusababisha ulemavu, kupoteza maisha na kudhoofisha uchumi wa nchi.


Pamoja na hayo, anasema katika kufikia lengo hilo, bidhaa hizo zinahitaji kuhakikiwa usalama, ubora na ufanisi kabla ya kuruhusiwa kutumika, na jukumu hilo linasimamiwa vizuri na Mamlaka hiyo.
Suala la udhibiti wa matangazo ya vyakula, dawa na vipodozi ni la kisheria na limeandaliwa chini ya Sheria Sura 219 na kwamba ilianza kutumika tangu mwaka 2010 na kwamba Mamlaka imeendelea kushuhudia sheria ikivujwa huku matangazo ya bidhaa yakitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari bila kibali cha TFDA, kinyume na matakwa ya sheria na kanuni na kuipotosha jamii.


“Pamoja na upungufu uliojitokeza, napenda kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari kwa TFDA, kwa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu upotoshaji wa matangazo unaofanywa na baadhi ya watu,” anasema.
Waziri Dk. Rashid anasema hivi karibuni TFDA ilitoa taarifa kuhusu uwepo wa dawa bandia zilizokuwa zimezagaa katika maduka ya dawa baridi nchini, na kwamba Serikali haitakuwa na huruma kwa wale watakaobainika kuwa na dawa hizo bandia.
Kwa mujibu wa waziri huyo, tunapaswa kuiangalia nchi yetu kwa kuhusisha tulikotoka, tulipo na twendako ili tuwe tofauti na nia za wanasiasa kwa lengo la kupotosha ukweli.


“Niliwahi kusema kwenye kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na Kituo cha ITV kwamba bahati mbaya linaona lakini lenyewe halijioni, hivyo tunapaswa kuwa wakweli kwa kuitangaza na kujivunia nchi yetu,” anasema Dk. Rashid.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Hiiti Sillo, amewashukuru wahariri wa vyombo vya habari kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mafunzo hayo na kuwa ni kielelezo cha ushirikiano mzuri uliopo kati ya vyombo vya habari na Mamlaka hiyo.
Sillo anasema TFDA ni wakala wa Serikali iliyoanzishwa chini ya kifungu namba 4 (1) cha Sheria namba 1 ya chakula, dawa na vipodozi sura 219 iliyoanza kutumika rasmi Julai 1, 2003.


Anasema Mamlaka hiyo imeanzishwa ili kuimarisha udhibiti wa usalama, ubora na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, lengo likiwa ni kuhakikisha bidhaa salama na zenye ubora unaokubalika ndizo zinazosambazwa na kutumika hapa nchini.
Licha ya makao makuu ya TFDA kuwa jijini Dar es Salaam, anasema wamesogeza karibu huduma kwa wananchi kwa kufungua ofisi kwenye kanda sita ambazo ni Mwanza (Kanda ya Ziwa), Arusha (Kaskazini), Mbeya (Nyanda za Juu Kusini), Dodoma (Kati), Dar es Salaam (Mashariki) na Mtwara (Kusini) na kwamba wanatarajia kufungua ofisi mkoani Kigoma kwa mikoa ya Kanda ya Magharibi katika mwaka wa fedha 2015-2016.


Sillo anasema Mamlaka hiyo imekasimu baadhi ya majukumu yake kwa halmashauri kupitia kanuni 2006 na marekebisho yake ya mwaka 2007 kwa lengo la kuongeza ufanisi wa udhibiti na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Hata hivyo, anasema wameanza utekelezaji wa mpango wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa kuwianisha mifumo ya udhibiti wa dawa (EAC Medicines Regulatory Harmonization Proramme) ambapo kuanzia Julai 2015, maombi yote ya usajili wa dawa yatakuwa na masharti yanayofanana kwa nchi zote tano za Jumuiya hiyo.


Kwa upande wake, Mwanasheria Mshauri wa TFDA, Iskari Fute, anasema kila mtu ana haki ya kukusanya na kutoa taarifa ikiwa ni moja ya haki za binadamu lakini zinapaswa kuwa za kweli.
Anasema usimamizi wa matangazo unapaswa kuzingatiwa kulingana na Katiba ya nchi. Wale wanaotangaza bidhaa zao katika vyombo vya habari ni lazima wawe na vibali kutoka TFDA ili kulinda afya za watumiaji.
“Kwa mfano, mtu hatakiwi kunywa dawa bila kupima uzito, lakini wanaotangaza dawa zao bila kuwa na vibali kutoka Mamlaka wanavunja sheria na kuhatarisha usalama na afya za walaji,” anasema.