Joseph MasikitikoTBSNovemba 10, 2015 Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Junus Ndaro, walizungumza na vyombo vya habari. 

Katika mazungumzo hayo, TEWUTA ilitoa salamu za pongezi kwa ushindi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, na Makamu wake kwa ushindi wao katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015. Pia TEWUTA ilitumia fursa hiyo kuelekeza tuhuma mbalimbali kwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Kutokana na hali hiyo, Menejimenti ya TTCL inapenda kuujulisha umma kuwa madai yaliyotolewa na TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL si sahihi.

Hoja za TEWUTA zimejikita katika upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL wenye nia na malengo ya kutekeleza mpango mkakati wa kuiboresha na kuiimarisha Kampuni ya Simu Tanzania.

Kwa uchache, Menejimenti ya TTCL inapenda kusema hali ya TTCL ni nzuri, utendaji wa kazi unaendelea vizuri, uhusiano wa kazi katika kampuni ni thabiti na jitihada mbalimbali za kuboresha huduma zinaendelea kwa ufanisi mkubwa. 

Menejimenti ya TTCL inasema hoja zote zilizotolewa na TEWUTA si za kweli, ni taarifa zilizopotoshwa kwa makusudi zikilenga kufanikisha malengo binafsi na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni, Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL wenye lengo la kuifanya kampuni kushamiri kibiashara na kutimiza kikamilifu wajibu wake kwa umma.

Muundo wa mishahara ya watumishi wa TTCL uko wazi na ndiyo unaotumika kulipa mishahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni ya Simu Tanzania.

Ofisi inayolipa mishahara ya wafanyakazi wote wa TTCL iko Idara ya Fedha na kusimamiwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu. Hakuna malipo yoyote ya siri yanayotumika tofauti na hayo yaliyoainishwa, hakuna posho zozote zinazolipwa kinyume na utaratibu.

Kwa kuzingatia mabadiliko ya kibiashara na soko la mawasiliano, Menejimenti iliomba na kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL kumtafuta mshauri mwelekezi kwa njia ya zabuni ili kupitia na kuishauri TTCL juu ya muundo mpya wa kampuni utakaoendana na mahitaji ya kibiashara na soko. 

Matokeo ya kazi hii ya mshauri mwelekezi yatabadilisha muundo wa kampuni, muundo wa mishahara na muundo wa utumishi wa Kampuni ya Simu Tanzania.

Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL imekuwa na mchango mkubwa sana katika kusukuma maendeleo ya TTCL chini ya uenyekiti wa Dk. Enos Bukuku na baadaye chini ya mwenyekiti wa muda, Jaji Joseph Warioba.

Mambo mengi yametekelezwa chini ya Bodi hii yakiwamo uendeshaji na usimamizi wa mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kuondoka kwa mbia mwenza, Bharti Airtel, utekelezaji wa mradi wa mabadiliko ya mfumo wa kibiashara (Transformation project) kusukuma jitihada mbalimbali za kuipatia kampuni mitaji ya kuiwezesha kufanikisha mipango yake kwa wakati.

Kampuni ya Rubiem ni mshauri mwelekezi aliyepatikana kwa kufuata taratibu sahihi za manunuzi ya umma. Mchango wa kampuni hii katika mpango wa mageuzi ya kibiashara ya kampuni ni mkubwa na unaonekana dhahiri. Matokeo ya kazi yake yataanza kuonekana mwishoni mwa mwaka huu ambapo huduma na bidhaa mpya zitaingia sokoni.

Mshauri huyu anatarajia kukamilisha kazi yake katika robo ya kwanza ya mwaka 2016. Ieleweke pia kwamba hatua ya Menejimenti kumuongezea muda mshauri huyu hazihusishi gharama zozote za nyongeza nje ya mkataba wake wa kazi na TTCL.

Kutokana na ufafanuzi huu, tunaomba umma kupokea taarifa hizi sahihi na kuendelea kuipa ushirikiano kampuni yao ya kizalendo ili iweze kuendelea kuwahudumia kwa ufanisi zaidi. Tunawahakikishia wateja wetu wote wa ndani na nje ya nchi kuwa tutaendelea kuwapa huduma bora zaidi, za uhakika na  kwa gharama nafuu.

 

Mwandishi wa makala hii Nicodemus Mushi, ni Meneja Uhusiano wa TTCL.