Tetemeko la ardhi linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa 4.8 katika kiwango cha Richter limeripotiwa kutokea mkoani Tanga.

Tetemeko hilo lililotokea takribani kilomita 33 kutoka usawa wa kisiwa cha Pemba jana Februari 08, 2023 lilipiga katika maeneo ya fukwe za Kayumbu Wete pamoja na Pemba.

Gabriel Mbogoni ambaye ni Mwandamizi wa Taasisi ya Jiolojia nchini amethibitisha kutokea kwa tetemeko hilo amesema kuwa tetemeko hilo limepiga katika nchi za Tanzania na Kenya ambazo zipo mwambao wa Bahari ya Hindi limetokea ikiwa ni siku tatu tangu litokee lile la Uturuki na Syria ambapo imearifiwa mpaka sasa zaidi ya watu 15,000 wamepoteza maisha.

Kwa nchini Tanzania si mara ya kwanza zilizala kama hiyo kutokea, itakumbukwa Septemba 10, 2016 mkoani Kagera tetemeko la ardhi lilitokea Bukoba likiwa na nguvu ya ukubwa wa 5.9 katika kipimo cha Richter ikiwa ni kilomita 40 chini ya uso wa ardhi.

Ni takribani watu 16 waliripotiwa kupoteza maisha na wengine 203 kujeruhiwa huku baadhi ya miundombinu kama vile shule nyumba na barabara ziliharibiwa.

Kulingana na tafiti za jiolojia tetemeko hutokea mara kwa mara japokuwa mengine huwa si rahisi kutambulika kikawada kwa binadamu bali vipimo vya kitaalamu.

Wataalamu wanaeleza kuwa tetemeko linaweza kutokea nchi kavu au hata baharini na mwambao wa pwani ambapo husababisha mawimbi makali ambayo huitwa Tsunami.

Endapo tetemeko kubwa litatokea wataalamu wanashauri mambo kadhaa ya kufuatilia ili kujikinga na madhara yatakayosababishwa na tetemeko husika kwa mfano vifo au hata majeraha kutokana na kuangukiwa na vitu vizito.

Hata hivyo inashauriwa kuwa kama upo ndani karibu na mlango palipotokea tetemeko la ardhi inashauriwa kukimbia haraka na kutoka nje ya jengo, endapo jengo hilo ni la ghorofa inashauriwa ushuke kutumia ngazi na siyo lifti na kama jengo ni imara basi unashauriwa kutulia ndani kwa tahadhari zaidi.

Endapo litatokea ghafala na hujui nini cha kufanya unashauriwa kukaa chini ya kitu kilichofunikwa kwa juu kama vile meza, jitahidi kushikilia meza hiyo isihame, pia hauko karibu na meza hakikisha unaziba kichwa kwa mikono yako miwili na usubiri mpaka litakapokwisha.

Pia likishatokea inashauriwa kutokimbia hovyo badala yake unatakiwa kutulia na kutoa taarifa kwa mamlaka za uokozi, ndugu na hata jamaa na pia kutogusa nyaya za umeme.