Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa magari ambayo yatatumika kusafirisha vitabu vya kiada na kuvisambaza katika halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam chini ya mpango mpya uliobuniwa na kuzinduliwa hivi karibuni na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Akizungumza katika tukio hilo fupi la uzinduzi wa usambazaji wa vitabu vya kiada na mwongozo wake; Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, ameishukuru JWTZ kwa kutoa magari hayo akisema yatasaidia sana kufanikisha mpango huo.
“Zoezi hili la usambazaji linaanza leo, ambalo litafanywa na watumishi wa TET na maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Hatutaishia hapa kwenye hivi vitabu, bali tutaendelea kuboresha zaidi, kwani mpaka sasa tumekwisha kusaini
mikataba mingine ya dola milioni 90 za Marekani ambayo itasaidia kupata vifaa vya kufundishia ngazi ya msingi, kutoa
mafunzo kwenye ngazi ya msingi na itasaidia kujenga madarasa. Pia Wizara ya Elimu tunazidi kujitahidi kuhakikisha shule zetu za serikali zinakuwa bora zaidi na kuwa mfano, kwani mpaka sasa watoto wanakuwa na ufaulu mzuri,” anasema Dk. Akwilapo wakati akizindua mpangp huo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TET, Aneth Kombo, amevitaja aina ya vitabu ambavyo vimezinduliwa kwa ajili ya kusambazwa shuleni.
“Vitabu vilivyopo ni vya darasa la sita, awali, kidato cha kwanza na pili na kidato cha tano na sita. Kazi ya uandishi
wa hivi vitabu vyote ilianza rasmi mwezi Februari mwaka jana na ilifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Elimu Tanzania na wataalamu wabobezi wa vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya ualimu, shule za msingi, wataalamu wastaafu na
hata wataalamu kutoka mashirika binafsi.