*Wananchi wadai kuna vivuko vinaendeshwa kama mali binafsi
*Abiria walazimika kumsubiri mkatisha tiketi kwanza apeleke fedha benki
DAR, UKEREWE
Na Waandishi Wetu
Baadhi ya watumiaji wa Kivuko cha MV Ujenzi kinachotoa huduma kati ya Kisorya, Bunda na Ngoma wilayani Ukerewe, wamelalamikia utaratibu mbovu wa ukataji tiketi na kutozwa gharama zaidi ya zilizopangwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa JAMHURI ambaye pia ni muathirika wa huduma za kivuko hiki, baadhi ya wananchi wamewatupia lawama Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Kanda ya Ziwa kwa kushindwa kusimamia wala kutatua malalamiko ya mara kwa mara wanayopeleka, wakiiomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuingilia kati.
“Kivuko vha MV Ujenzi ni cha serikali lakini kwa namna kinavyoendeshwa unaweza kufikiria kuwa ni mali ya mtu binafsi,” anasema Jumanne Magiri, mkazi wa Mugumu, Serengeti mkoani Mara.
Magiri ametoa mfano wa Aprili 20, mwaka huu alipovuka kwenda Ukerewe ambapo kwa muda mrefu yeye na abiria wengine hawakupata huduma kwa madai kuwa mkatisha tiketi ni mmoja tu, na anazunguka na kivuko.
“Wakati ninarudi, yaani Aprili 21, mwaka huu, nilifika saa tano asubuhi kivuko kikiwa Kisorya. Nikaegesha gari langu na kuanza kusubiri.
“Kivuko kilipofika, tukapanga mstari, lakini mkatishaji (anamtaja jina) hakuwapo mpaka iliposalia nusu saa ndipo akaingia. Ajabu, sisi tuliokuwa kwenye mstari hatukuhudumiwa kwanza, badala yake wengine wenye magari waliofika mwisho, ndio wakapata tiketi wa kwanza,” amesema na kuongeza:
“Nilipohoji ni wapi waliofika mwisho walikopata tiketi kabla yetu tuliokuwa kwenye mstari, mhudumu huyo akanishambulia kwa matusi, akisema nimelewa. Nikawatafuta maofisa wengine kutaka kujua utaratibu gani unaotumika na sababu za mimi kutukanwa, sikupata msaada wowote.”
Magiri amesema kilichoonekana ni kuwa baadhi ya watumishi huwasiliana na wenye mabasi na malori ya mizigo nje ya utaratibu uliowekwa, hivyo kuwaathiri watu wanaovuka kwa mara ya kwanza na wenye magari madogo.
Anaiomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuwafuatilia watendaji wa kivuko hicho akidai kuwa mazingira yanaonyesha kuna fedha haziingii serikalini, hivyo kuitia hasara serikali.
Abiria mwingine aliyekuwa akitokea Nansio kwenda Bunda siku hiyo hiyo, Vedastus Makaranga, amelalamikia kuwapo kwa tofauti ya nauli.
“Hapa nauli ni Sh 400, lakini nimetozwa Sh 500, nikaandikiwa kuwa nina baiskeli. Nilipouliza sababu za kunitoza chombo ambacho sikimiliki, mkatishaji akawa mkali kabisa. Katika mazingira hayo, kuna watu wengi watakuwa wanaonewa na hawasemi,” amesema.
Mmoja wa abiria (jina limehifadhiwa) amesema baadhi ya madereva au wamiliki wa mabasi na malori yanayosomba machungwa wana uhusiano fulani na maofisa wa kivuko.
“Ndiyo maana wao hata wakichelewa kufika wanakuwa wa kwanza kupanda kivuko. Hata bosi wa wahudumu wa hapa ameshaambiwa lakini hajali. Akifika hapa anakwenda kutazama mbuzi (mifugo) wake tu,” amesema.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa awali kulikuwapo mashine mbili za kukatia tiketi na hakukuwa na usumbufu hata kidogo.
Mmoja wa wafanyakazi ameliambia JAMHURI akisema: “Wakubwa walikuja wakaondoa mashine moja. Kwa hiyo mkatisha tiketi anapomaliza, huondoka na kivuko hadi upande wa pili. Akifika, kwanza anapeleka fedha benki ndipo arudi kuwakatia tiketi abiria wengine.”
Mbali na hilo, wafanyakazi wa TEMESA wa Kivuko cha MV Ujenzi wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo kutokuwapo mfumo mzuri wa udhibiti mapato, tofauti na vivuko vinavyomilikiwa na watu binafsi.
TEMESA wakiri matatizo
Meneja wa Wakala wa TEMESA (Vivuko) Kanda ya Ziwa, Julius Humbe, ameliambia JAMHURI na kukiri kuwapo kwa tatizo la mkatishaji wa tiketi.
“Hili tatizo si kivuko hicho pekee, lipo maeneo mengine pia. Sababu kubwa ni upungufu wa watumishi. Lakini ninaahidi kulishughulikia haraka suala hili na kuondoa usumbufu na msongamano unaosababisha migogoro kama hiyo,” amesema.
Humbe pia ameahidi kufuatilia na kushughulikia malalamiko yote kutoka kwa wananchi, akiwamo abiria kutukanwa na mtoa huduma, kukatisha tiketi tofauti na bei elekezi na: “Hili la mashine, lazima tutaongeza mara moja ili kuwepo na mtu wa kukatisha tiketi kila upande wa kivuko.”
Kuhusu mabasi kupewa kipaumbele, Meneja Humbe anasema amaewahi kuuliza na kuelezwa kuwa kumewahi kutolewa tamko la upendeleo kwa mabasi, ingawa hajui ni nani aliyetoa.
Hata hivyo, anakiri kuwa kivuko hicho ni kidogo sana wakati mwingine magari yakiwa mengi hulazimika kusubiri kwa muda mrefu.
“Kama ni ‘semi trela’ linaweza kusubiri hata siku mbili kabla ya kuvushwa peke yake. Hizo ni changamoto zinazotukabili,” amesema.
Malalamiko ya Dar es Salaam
Kwa upande mwingine, wakazi wa Kigamboni na watumiaji wengine wa kivuko cha Magogoni jijini Dar es Salaam nao wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu kwa TEMESA na maofisa wanaotoa huduma eneo hilo.
Hali hiyo inatokana na uamuzi wa serikali kuweka utaratibu wa kutumia kadi za kielektroniki, huku ikibainika kuwa idadi kubwa ya abiria, wengi wakiwa ni wakazi wa Kigamboni, hawana kadi hizo.
Wiki kadhaa zilizopita JAMHURI limeshuhudia watu wachache wanaomiliki kadi wakizitumia kuwavusha wengine baada ya kupewa Sh 200 kwa safari moja.
“Sababu kubwa ni kwamba wengi hatuna uwezo wa kumudu gharama za kadi. Mimi tangu utaratibu huu ulipoanza sijawahi kununua kadi. Kipato changu ndicho hicho, Sh 200 ninayo, ninapata kila siku, lakini sina uwezo wa kununua kadi na kuijaza fedha kila mara,” anasema Salumu Nassor, abiria aliyezungumza na JAMHURI upande wa Kigamboni.
Nassor ni mmoja wa abiria walioshuhudiwa na JAMHURI akitoa Sh 200 kwa mmiliki wa kadi na kuvushwa getini kwenda kupanda kivuko.
Gharama ya kadi hiyo ni Sh 1,000 na hutakiwa kujazwa fedha kiasi chochote kuanzia Sh 1,000; kiwango ambacho Nassor anasema ni kikubwa kutolewa na mtu kama yeye kwa pamoja kwa ajili ya usafiri.
Amesema kazi anayoifanya kwa kutwa humwingizia fedha zinazotosha kula yeye, familia yake na nauli yake ya siku moja tu pamoja na ya watoto kwenda shule.
“Tunaomba serikali ituangalie watu wa hali ya chini na kurudisha mfumo wa zamani wa kulipa Sh 200 kisha unapewa tiketi. Hii itatusaidia, kwa kuwa kwa sasa mtu unachelewa kuvuka kwa kumsubiri mmiliki wa kadi mwenye roho nzuri akubali kukusaidia kukupitisha getini,” amesema.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Nassor, mwananchi mwingine, Bahati Amran, anaufurahia utaratibu wa kutumia kadi za kielektroniki akisema zimeondoa foleni.
“Ni vigumu kujua umuhimu wake, lakini kwetu wafanyakazi unasaidia sana kuwahi kazini kuliko ilivyokuwa awali. Sijui kwa nini mwendokasi (mabasi yaendayo haraka) hawatumii mfumo huu,” anasema Bahati.
Ofisa Habari wa TEMESA, Alfred Mgweno, amesema lengo la wakala hao wa serikali ni kuhakikisha kila mtu anatumia kadi hizo ili kuboresha makusanyo.
“Hii kadi ya kisasa ina faida kubwa kwa kuwa mmiliki wake anaweza kuitumia kuingia hata mpirani, pia kulipia bidhaa super market.
“Lakini kwa sasa bado kuna kadi za dharura za malipo ya Sh 200 kwa wale wasiotumia kivuko mara kwa mara. Baadaye huduma hii tutaiondoa kabisa,” amesema Mgweno.
Habari hii imeandikwa na Anthony Mayunga (Ukerewe) na Aziza Nangwa (Dar es Salaam)