Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amependekeza TEMESA itathmini mikakati mbadala ya kupunguza utegemezi wa vivuko vya mwendokasi kwa kuwa kuendelea kukodisha vivuko hivyo kutoka Kampuni ya Azam Marine kunaathiri uendelevu wa huduma ambapo TEMESA inailipa Azam ada ya huduma kila siku Tsh. milioni 5 pamoja na kodi ya zuio ya asilimia 5.
Kupitia Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, CAG amesema “June 14, 2022, Wakala wa Huduma za Umeme Tanzania (TEMESA) uliingia mkataba wa makubaliano (MoU) na Kampuni ya AZAM Marine Ltd ya kukodi na kuendesha vivuko viwili vya baharini ‘Sea Taxi 1’, na ‘Sea Taxi 2’ kati ya Magogoni na Kigamboni, mpango huu ulilenga kuongeza uwezo wa TEMESA kuhudumia Wateja kufuatia ukarabati mkubwa wa Kivuko cha MV Magogoni”
“Kila kivuko kilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 250 kwa kila safari, kwa mujibu wa Kifungu Na. 5 cha Mkataba wa Makubaliano, mkodishwaji (TEMESA ), analazimika kuilipa Kampuni ya AZAM Marine Ltd ada ya huduma kila siku ya Sh. milioni 5 (pamoja na kodi ya ongezeko la thamani) pamoja na kodi ya zuio ya asilimia 5, Mkodishaji, Kampuni ya AZAM Marine itatoa ankara ya malipo kila mwezi inayoeleza idadi ya siku ambazo huduma ilitolewa kwa mkodishwaji katika mwezi husika.
“Nilibaini kuwa kuanzia Julai 1, 2022 hadi June 30, 2023, TEMESA ilikusanya jumla ya Sh. bilioni 5.76 za tozo za vivuko katika Kituo cha Magogoni – Kigamboni, kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 1.83 (sawa na asilimia 31 ya makusanyo yote) zililipwa kwa Kampuni ya AZAM kwa ajili ya uendeshaji wa vivuko viwili”
“TEMESA ilibakiwa na Sh. bilioni 3.93 (asilimia 69) ili kulipia gharama za undeshaji kama vile mafuta ya vivuko, gharama za kazi, ukarabati na matengenezo, na gharama zinginezo, hata hivyo, kiasi kilichobaki cha Sh. bilioni 3.93 kilikuwa hakitoshi kulipa gharama hizo, hivyo kusababisha Wakala wa Huduma za Umeme Tanzania kutumia fedha za vyanzo vingine kugharamia undeshaji wa kituo cha Magogoni – Kigamboni, hali hii inasabisha Wakala kuendelea kutegemea ruzuku ya serikali kugharamia shughuli zake badala ya kujitegemea, napendekeza TEMESA iongeze idadi ya vivuko ili kukabiliana na ongezeko la Wateja”