Uchumi
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji, Elde Kimaro, akiongelea shughuli za kilimo ndani ya Manispaa anasema Temeke ina eneo lenye ukubwa wa hekta 65,600, kati ya hizo hekta 45,000 zinafaa kwa shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali.
Amesema wakazi wengi maeneo ya Temeke hulima mazao ya mbogamboga ambapo hutumia kilimo cha magorofani, kilimo hiki ni cha kutumia eneo dogo kwa kutumia viroba, chupa za maji ama maboksi ya mbao.
Hata hivyo, JAMHURI limebaini kuwa ufugaji nyuki unatekelezwa na watu wasiopungua 40 na vikundi visivyopungua vitatu. Vikundi hivyo ni pamoja na vikundi vya Kibugumo na Vikuruti. Hadi sasa jumla ya mizinga 173 inamilikiwa na vikundi hivyo na kiasi cha lita 150 za asali zimevunwa msimu huu yenye thamani ya milioni 1.5.
Afisa Uchumi na Mipango Temeke, Mariam Madalu, amesema; “Tumepanga maeneo manane kwa ajili ya uwekezaji, ambayo tayari yameendelezwa. Nayo ni Mkuki House, jengo la kibiashara lililopo kwenye kiwanja chetu kilichoko Ilala karibu na Nakumatt, mradi huu ni wa ushirika kati ya Manispaa na kampuni ya Show Max kutoka Dubai. Maeneo mengine ni Temeke Mwisho, eneo palipokuwapo na nyumba za kota, ambako tumeanza utekelezaji wa ujenzi wa soko la kimataifa la bidhaa za zote.”
Ajira
Manispaa ya Temeke imefanya makubaliano maalumu na Benki ya DCB Commercial Bank Plc ya kusimamia fedha kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana. Mkurugenzi wa DCB Commercial Bank Plc, Edmund Mkwawa, amesema asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri yatakuwa yakitumwa kwenda benki hiyo ili kufanikisha azma ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo.
Amesema mpaka sasa Manispaa imekwishapeleka sh milioni 600 kati ya bilioni 5 zinazokusudiwa kuwekwa ifikapo mwaka 2020, ili ziweze kutumika kwa kukopesha vikundi vya wanawake na vijana kwa Manispaa za Temeke na Kigamboni baada ya kugawanyishwa.
“Faida ambazo wajasiriamali watapata ni kuwa hakuna ulazima wa kusajili kikundi hicho bali watadhaminiana wao wenyewe na Benki ya DCB itapunguza riba kufikia asilimia 10,” anasema Mkwawa.
Changamoto
Palipo na mafanikio hapakosi changamoto. Mkurugenzi wa Manispaa Temeke, Mbaga, amesema kuwa wana tatizo la uhaba wa walimu hasa masomo ya sayansi katika shule za sekondari na uhaba wa vifaa vya kufundishia masoma hayo.
Changamoto nyingine ni gharama kubwa ya uendeshaji wa shughuli za kuzoa taka kutokana na taka zote za jiji kutakiwa kupelekwa dambo la Pugu, kama km 20 kutoka Temeke, na nyingine ni ukosefu wa maeneo ya kutosha kujenga shule hasa mijini ambayo huhitaji fidia kubwa kuyatwaa.
Mikakati Endelevu
Manispaa ya Temeke imejipanga kuimarisha zaidi ushirikiano na wadau wote katika kupambana na umaskini hususani katika kutoa elimu na mikopo mingi zaidi kwa sekta inayojiajiri, ambayo ina uwezo wa kutengeneza ajira kwa vijana wengi, na kuhamasisha matumizi endelevu ya maliasili ikiwamo matumizi endelevu ya ardhi hasa uratibu wa maendeleo ya makazi yasiyopimwa.
Kuendelea na uhamasishaji na uundaji wa vyama vipya vya kuweka na kukopa makazini na viwandani, kama silaha muhimu dhidi ya umaskini na kuboresha mbinu za kushughulikia kero za wananchi kwa kuanzisha dawati la upokeaji kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi.
>>TAMATI