Machafuko ya kisiasa katika nchi za Afrika na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, kumechangia kuzagaa kwa silaha za kivita katika baadhi ya nchi ikiwamo Tanzania, hatua iliyotajwa kuwa kichocheo kikubwa cha mauaji ya tembo nchini.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Tembo Duniani (World Elephant Centre), Dk. Alfred Kikoti, katika mkutano wa mwaka wa hifadhi za Taifa uliowakutanisha wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo mbali mbali vya habari nchini.
Mkutano huo uliofanyika mjini Morogoro kwa siku tatu, uliandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na kufunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, huku ukibeba kaulimbiu ya ‘Tuzilinde hifadhi za Taifa ili kukuza uchumi wa Taifa.’
Dk. Kikoti, mtafiti wa tembo na faru, anasema kuzagaa kwa silaha kumechangia silaha nyingi kuingia kwenye mikono isiyo salama yakiwamo makundi ya kigaidi ya al-Shabaab linaloendesha mapigano katika nchi ya Somalia.
Mapigano katika nchi ya Somalia yaliyodumu kwa kipindi kirefu baina ya wanamgambo hao wa al-Shabaab, yamechangia kwa kiasi kikubwa kuzagaa kwa silaha nyingi za kivita kutokana na kutokuwapo kwa udhibiti wowote.
Dk. Kikoti amesema kuwa migogoro iliyoikumba nchi jirani ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia wa Kongo (DRC), Sudan Kusini na Uganda imekuwa kichocheo ya kuzagaa kwa silaha zinazohatarisha usalama wa tembo nchini.
Anasema kama hatua madhubuti hazitachukuliwa, kuwalinda tembo na faru, utalii utatoweka.
Anabainisha kuwa soko la tembo limepanuka hata kwa nchini ambazo zilikuwa hazijihusishi na biashara hiyo, ikiwamo Nigeria ambako pembe hizo za tembo zinauzwa kama nguo sokoni.
Nchi nyingine zilizotajwa katika soko la uuzwaji wa pembe za tembo duniani ni China, Marekani, Hong Kong, Thailand, Ethiopia, Japan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), India, Singapore, Vietnam, Kenya na nchi za Bara la Asia, ambako uuzwaji wake hufanywa kwa uwazi bila kificho.
Dk. Kikoti anaeleza kuwa miaka mitano iliyopita idadi ya tembo hapa nchini ilipungua kwa kiwango cha asilimia 60 kutoka tembo 109,051 mwaka 2009 na kufikia tembo 50,000 mwaka 2014.
Anasema kuwa ni lazima jamii ishirikishwe kuhakikisha inawalinda tembo na faru kutokana na kuwa katika tishio la kutoweka kutokana na kuwindwa na majangili.
Tishio jingine la kutoweka kwa tembo ni kuvamiwa kwa mapito yao ya asili maarufu kama ‘shoroba’ kulikotokana na shughuli za kibinadamu, hatua ambayo imesababisha mgongano mkubwa baina ya wanyama na binadamu.
Dk. Maurus Msuha kutoka TAWIRI anasema migogoro baina ya wanyama na binadamu inazidi kuongezeka, huku shoroba zikitumiwa na wananchi kwa ajili ya kuweka mitego ya kunasa wanyama.
Dk. Msuha anasema umuhimu wa kuwapo na shoroba ni kuwawezesha wanyama kupita kutoka eneo moja kwenda jingine bila bughudha, huku akiitaja Tanzania kama nchi ya sita duniani yenye viumbe walioko hatarini kutoweka.
Hifadhi ya Taifa ya Tarangire iliyoanzishwa mwaka 1970 kwa tangazo la Serikali namba 160, ni moja ya hifadhi ambazo mapito ya wanyama yamevamiwa kwa kiwango kikubwa huku kukiwapo na tishio la kutoweka kwa nyumbu.
Mbali na shoroba hizo kuvamiwa, pia Mto Tarangire unaobeba jina la hifadhi hiyo, nao upo hatarini kutoweka kutokana na shughuli za kibinadamu zinazochangia uvamizi wa vyanzo vya maji ndani ya mto huo.
Dk. Msuha anasema kuwa shoroba nyingine zilizovamiwa ni; Manyara-Ngorongoro, Tarangire-Manyara (kwa kuchinja), Tarangire-Simanjiro, Kilimanjaro-Amboseli (Kenya), Udzungwa-Ruaha, Udzungwa-Selous, Gombe-Kwitanga, Gombe-Mukungu-Rukamabasi, Katavi-Mahale, Katavi-Rukwa-Lukweti na Saadani-Wami mbiki.
Dk. Msuha anasema kuwa zipo shoroba tano zilizoko katika hatari ya kutoweka kabisa, kutokana na kuvamiwa na wananchi wanaoendesha shughuli za kibinadamu ikiwamo kilimo na ufugaji.