Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Sengerema
Hali ya usalama wa maisha ya kila siku kwa wananchi waishio pembezoni mwa ziwa Viktoria wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza yarejea baada ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kujenga vizimba vya kudhibiti mamba.
Akizungumza na vyombo vya habari, Mtafiti wa Mamba kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt.Iddi Lipende ambaye pia ni Daktari wa Wanyamapori amesema, Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutatua migongano kati ya binadamu na Mamba kwa kutenga bajeti ya kujenga vizimba vya mfano, ambapo mpaka sasa Wizara imewezesha ujenzi wa jumla ya vizimba sita (06) nchini na kati ya vizimba hivyo vinne (04) vimejengwa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.
Dkt. Lipende amesema, matumizi mazuri ya vizimba vya kuzuia athari za mamba yameonyesha ufanisi mkubwa katika kuzuia na kupunguza athari za mashambulizi ya mamba kwa wananchi ambapo tafiti zilionyesha athari zilikuwa zikiwapata wanaotumia maji ya ziwa au mito kwa matumizi ya nyumbani kama kuchota maji, kuosha vyombo, kufua na kuoga.
” Kundi la wananchi lililokuwa likiathirika zaidi na Mamba ni wanawake na watoto” amesema” Dkt. Lipende
Vilevile, Dkt.Lipende amebainisha kila kizimba kimoja kina ukubwa wa upana wa mita 30 na urefu wa 35 ambapo mita 20 za uzio zipo ndani ya maji na Mita 15 zipo nchi kavu, hivyo kutoa nafasi kwa jamii kutumia eneo hilo kwa uhuru na usalama kwani uzio hutenganisha watu na mamba.
“Pamoja na ujenzi wa vizimba hivi, jamii haina budi kufanya uangalizi wa karibu kwa watoto “amehimiza Dkt.Lipende
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Asenyi Ngaga ametoa wito kwa wanachi kutumia vizimba hivyo kwani licha ya Serikali kuvijenga bado kuna changamoto ya baadhi ya wananchi kuendelea na mazoea ya kuendelea kuoga nje ya maeneo ya vizimba, tabia ambayo huatarisha usalama wa maisha yao
“Hatupendi kuona watu wanapotea ndio maana tunawakumbusha wananchi wetu kuendelea kuchukua tahadhari kwa kutumia vizimba hivi” amehimiza Mhe. Ngaga
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wananchi wa Kijiji cha Nyakaliro, Halmashauri ya Buchosa wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Vizimba hivyo ambapo wamekiri kurejesha amani na furaha kwani vinawasaidia kuwahakikishia usalama na kuendelea na shughuli zao za kijamii kama kawaida.
“Mwanzoni tulikuwa na shida kubwa sana ya mamba, watu walikuwa wanakamatwa watoto wanakufa kwa ajili ya mamba lakini kutokana na hiki kizimba amani imerejea, tunaishukuru Wizara ya Maliasili na taasisi zake za TAWIRI na TAWA kwa kutujengea hiki kizimba amesema” Elizabeth John Mkazi wa Kijiji cha Nyakaliro.
Nae, Beatus Maganja kutoka TAWA, amesema kuanzia Julai 2023 hadi Mei 2024 TAWA ilifanya jumla ya mikutano 84 ya kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu mbalimbali za kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko katika vijiji 44 na shule 40 ambapo jumla ya watu 53,639 walifikiwa na elimu hiyo
Ikumbukwe, ujenzi huu wa vizimba vya jamii vya kuzuia mamba umefadhiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori (TWPF) na TAWA amba vizimba hivyo sita (06) vya mfano vimejengwa katika Vijiji vya Kanyala, Izindabo, Nyakaliro na Nyachitare wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza na vizimba vinne vimejengwa Rukwa na Iboma wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe.