Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia kuanza kufanya upasuaji wa ubongo kwa kutumia mawimbi ya sauti.

Hatua hiyo inaifanya hospitali hiyo kuwa ya kwanza kwa nchi Kusini mwa Jangwa la Sahara kutumia teknolojia hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk Mpoki Ulisubisya ametoa taarifa hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya awamu ya nne ya magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu katika ukumbi wa mikutano wa Ummy Mwalimu uliopo Hospitali ya Taifa Muhimbili- Upanga.

Dk Mpoki amesema teknolojia hiyo itasaidia kufungua sehemu ndogo ya kichwa na kumuacha mgonjwa na kovu dogo.

“Huu utaalam wa kutumia mawimbi ya sauti kufuatilia maendeleo ya upasuaji kwa watu (wagonjwa) ambao wana uvimbe ndani ya ubongo, uwe wa saratani au wa namna nyingine ni wa kwanza Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa hiyo sisi (MOI) tunaongoza… Nachelea kusema wengine watafuata na wataalam wetu watatumika kama walim kwa wanafunzi wanaotoka nchi za Afrika Mashariki na Kati na wengine wataopata nafasi ya kutembelea nchi yetu (Tanzania) kwa ajili ya afua hizi,”

“Maana yake tunaweza kusema mtu yeyote anayekuja hapa Tanzania mwenye changamoto kama hiyo ujuzi huo (teknolojia ya upasuaji wa ubongo kwa kutumia mawimbi ya sauti ndio utakaotumika kumtibu, miaka yote sisi (MOI) tutakuwa mbele,” amesema Dk Mpoki.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI, Dk Laurent Lemeri Mchome amesema kuwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani na MOI ulianza tangia mwaka 2013 ambapo wataalam kutoka Marekani walitembelea MOI na kukuta wataalam wa MOI wanafanya upasuaji kwa kufungua kichwa.

Kwa upande wake, Daktari bingwa mbobezi wa Ubongo, kutoka Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani, Dk Rayn Ormond ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa idhini na kibali cha kuendesha mafunzo hayo nchini Tanzania.

Mafunzo hayo yameanza leo Jumatano Februari 17 na yatafikia tamati Februari 21, 2025 na yameandaliwa na kuratibiwa na MOI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani ambapo wataalam kutoka MOI, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Bugando, Hospitali ya Rufaa Kanda- Mbeya, Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila, Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH)- Dodoma na Lugalo wamehudhuria.