Mhariri Mtendaji wa Gazeti JAMHURI, Deodatus Balile, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Balile alichaguliwa katika nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi iliyopita mjini Morogoro.

Katika uchaguzi huo uliojaa ushindani, Balile alipata kura 47 na kumshinda Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu, aliyepata kura 17 kati ya kura 64 zilizopigwa. 

Afisa Mtendaji wa Kampuni ya Jambo Concept, Theophil Makunga, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya. Makunga aliyepata kura 34 kwa upande wake, alimshinda Jesse Kwayu aliyevuna kura 32 katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Mratibu wa TEF, Prisca Kabendera.

Nafasi ya Katibu wa Jukwaa la Wahariri itaendelea kushikiliwa na Mhariri Mtendaji wa Free Media Ltd, Neville Meena, aliyepita bila kupingwa. Katibu Msaidizi ni Negda Johanes.

Wajumbe wa bodi ya TEF ni pamoja na Salim Said Salim kutoka Zanzibar; Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Jesse Kwayu; Mhariri wa Clouds Television, Joyce Shebe; Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu, na Mhariri wa Mwananchi, Lilian Tumbuka.