Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa kauli ya Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kuwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016) umeshindikana kuingizwa bungeni kutokana na ripoti nyingi za Kamati za Kisekta za Bunge.
TEF inaona sababu iliyotolewa ni nyepesi na inapata wasiwasi iwapo kuna utashi wa kufanya mabadiliko katika sheria hii. Katika vikao vilivyotangulia, tumeuona ugumu kutoka kwa baadhi ya maofisa wastaafu walioazimwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), maafisa kutoka
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, na baadhi ya vyombo vya ulinzi na usalama wakionesha wazi kutokuwa na nia ya kurekebisha sheria hii.
Mara kadhaa vikao tulivyofanya, viliisha bila mwafaka katika vifungu mbalimbali ikiwamo Mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) chini ya vifungu vya 9 na 10, ambavyo vinampa mamlaka ya kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, mtoa hukumu na msimamizi wa utekelezaji wa hukumu; suala tunalosema ni ukiukwaji wa Utawala Bora na Utawala wa Sheria.
Taaluma nyingine nchini, mabaraza yake au bodi zake ndizo zinazofanya kazi hii, ila maafisa hawa wachache, wanang’ang’ania sekta ya habari madaraka haya yawe katika mikono ya mtu mmoja; Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), suala tunalosema halikubaliki.
Ilituchukua hadi kikao cha Novemba 21, 2022 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alipolazimika kusimamia kikao hicho ndipo maafisa hao watatu wakakubali kwa shingo upande kusema watarekebisha vifungu hivyo ili viendane na viwango vya kimataifa.
Kinachotushangaza, baadhi ya vifungu wanavyoving’ang’ania kama kashfa kugezwa jinai, tayari vimefutwa kwenye sheria mama ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.
Tumekuwa na mawasiliano mazuri na Waziri Nape; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk. Eliezer Feleshi; Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Serikali, Onorius Njole; na Ofisi ya Bunge, ila maafisa wachache wa chini ndiyo kwa muda mrefu wamekwamisha mabadiliko ya sheria hii.
Mwanzo tuliahidiwa muswada wa mabadiliko ungeingizwa bungeni mwaka 2022 katika vikao vya Februari,wakasema Aprili, baadaye Septemba, ikasogezwa Novemba, lakini kote huko hakuna kilichotekelezwa.
Zamu hii tuliweka matumaini makubwa na hasa baada ya Waziri Nape kutangaza hadharani kuwa amewasilisha mapendekezo ofisini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwa Februari hii muswada huu ungeingizwa bungeni.
Kwa namna ya ajabu, muswada huu umeshindikana kuingia bungeni tena (Februari, 2023). Tunajiuliza kama taarifa za kamati zimezuia muswada kuingia bungeni, je, muswada huu utapataje nafasi kwenye mkutano ujao wa Aprili, 2023? Je, itawezekana vipi katikati ya hotuba za Bunge la Bajeti la mwaka 2023/2024?
Suala la kubadili sheria hii limekaa muda mrefu. Sisi tunapodai Uhuru wa Habari si kwa sababu ya wanahabari pekee, hapana. Uhuru huu ni wa Watanzania wote kutoa maoni yao; na kwa kufanya hivyo tunakuza demokrasia nchini na kuongeza uwajibikaji.
Ni kawaida watu wenye shaka na watendayo, huwa hawataki mambo yao yafahamike mbele ya jamii, hivyo njia pekee na rahisi ni kukandamiza vyombo vya habari visiwe huru kusema ukweli bila upendeleo wala uonevu.
Kwa kuwa Juni 28, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza TEF na wadau tukakae na Wizara inayosimamia habari tuzungumze jinsi ya kubadili sheria hii ili ikidhi viwango vya kimataifa; na kwa kuwa alisema tukikwama sehemu yoyote au tukashindwa kuelewana tusisite kurudi kwake, basi tunaomba Mhe. Rais Samia atupe nafasi ya kukutana naye tumweleze wapi tumekwama na
wanaokwamisha ni kina nani, pengine akiwauliza yeye watampa majibu ya msingi kuliko tunavyoshuhudia wakitupuuza sisi kwenye vikao.
Jukwaa la Wahariri na Wadau, kwa kuona kazi kubwa anayoifanya Rais Samia ya kurejesha uhuru katika sehemu mbalimbali nchini ikiwamo kufungulia magazeti ya Mwanahalisi, Mseto, Tanzania Daima na Mawio, kurejesha Bunge Live, kushusha bei za leseni za TV na Radio, tuliamini njia ya diplomasia ingetufikisha katika nchi ya ahadi, ila tunaona baadhi ya maafisa hawako tayari kuona uhuru wa habari ukirejea nchini.Tunaomba Rais Samia anusuru hali hii.
Hatujafurahishwa na danadana tunazopigwa katika suala la mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016).Tunaomba tukutane na Mhe. Rais Samia, tukiamini mkutano huo utatukwamua tulipokwama.
Mungu ibariki Tanzania.