Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa kuona umuhimu wa kupitia sheria za habari na kuagiza zifanyiwe maboreshio ili kuendana na mazingira yaliyopo.
Hayo amesema leo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na kituo cha Radio One ambapo alikua anatoa ufafanuzi kuhusu kikao cha majadiliano ya mabadiliko ya sheria kati Serikali kupitia Wizara ya habari na wadau wa habari kitakachofanyika kesho Agosti 11,mwaka huu, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Balile amesema kuwa wadau wa habari wanapodai mabadiliko ya sheria hawataki huruma na upendeleo bali wanataka wajibu na haki kama ilivyo kwenye taaluma nyingine.
Akitolea mfao wa kifungu kimojawapo ambacho wadau wa habari wanakilalamikia Balile amesema mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) kwenye Kifungu cha Tisa ya kufungia au kufuta leseni ya gazeti haijakaa sawa kwa sababu anaweza kufanya hivyo endapo gazeti husika litaandika habari za kuikosoa Serikali.
Akizungumzia mwendeno wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya Balile amesema Taifa hilo limepiga hatua kubwa kwa namna ambavyo yamefanyika na mchakato wa kutangaza matokeo umekua na uwazi, hivyo ameshauri Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 nchini Tanzania ufanyike kwa viwango bora.
Amesema vyombo vya habari vya Kenya vinarusha mubashara hadi kura zinavyohesabiwa kitu ambacho huwezi kukiona kwenye Uchaguzi Mkuu wa hapa Tanzania.
” Vyombo vya habari vya Tanzania vipewe ruhusa ya kuingia hadi kwenye vituo vya kupigia kura kurusha Mubashara kwasababu kinachofanyika ni uhalisia hivyo hakuna haja ya kuficha kila kitu kifanyike kwa uwazi” amesema Balile.