Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na baadaye, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luteni Yusuf Makamba, alipata kusema hivi: “Mti wenye matunda ndiyo unaorushiwa mawe.”
Wiki iliyopita nimethibitisha kauli ya Luteni Makamba. Nimeithibitisha baada ya kutia saini tamko la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa wadhifa wangu kama Makamu Mwenyekiti wa TEF, lililoikumbusha jamii kuwa Televisheni ya Star imeamua kujitangaza kama adui wa vyombo vya habari kwa kutangaza nia ya kuhojiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Sitanii, naandika makala hii siku mbili kabla ya Jumatatu. Sina uhakika kama Star TV wataendelea na mpango wao wa kuhojiana na Makonda au la, ila kwa nia ya kuwa na uelewa unaofanana, naomba niliweke hapa chini, tamko tulilotoa kuwaasa Star TV wasifanye hivyo kwa nia njema, badala yake likaibua tuhuma dhidi ya TEF na viongozi wake kupitia mitandao ya kijamii, tuhuma ambazo nazo nitaziweka na kuzitolea majibu.
Tamko:
UAMUZI WA STAR TV NI USALITI KWA TAALUMA YA HABARI
Kwa muda wa wiki moja sasa kampuni ya Sahara Communications Limited, wamiliki wa Star TV na vyombo vingine vya habari kupitia mitandao ya kijamii, wanasambaza taarifa kuwa watafanya mahojiano maalumu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Jumatatu Mei 22, 2017.
Kusudio hilo la Star TV limekuja wakati kiongozi huyo akiwa amefungiwa na vyombo vya habari, kwa uamuzi uliofikiwa kwa pamoja baina ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kuungwa mkono na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) na taasisi nyingine za kihabari nchini. Uamuzi wa kumfungia Makonda uliotangazwa Machi [22], 2017, ulitokana na kiongozi huyo kuvamia Kituo cha Utangazaji cha Clouds, Machi 17, 2017 akiwa na askari wenye bunduki.
Uvamizi wa Clouds ulikuwa mwendelezo wa matukio ya RC Makonda kudhalilisha wanahabari, kutukana na kutoiheshimu taaluma ya habari. Katika tamko hilo, Makonda tulimpa masharti mepesi kurejesha uhusiano na tasnia ya habari, ambayo ni kuomba radhi waandishi wa habari kwa tukio la Clouds na matukio mengine kwa ujumla wake kama sehemu ya uungwana wa Kitanzania.
Tulisema katika tamko hilo, kuwa yeyote atakayeshirikiana na Makonda [kabla hajaomba radhi] naye tutamhesabu kama adui wa tasnia ya habari nchini. Kwa mantiki hiyo tunasema ikiwa Star TV wameamua kushirikiana na Makonda, basi ni wazi wameamua kwa hiyari yao wenyewe kujitangaza kama adui wa tasnia ya habari nchini. Kila Mtanzania anajua jinsi ya kupambana na adui kwa nia ya kujilinda, na tasnia haitasita kufanya hivyo.
Kadhalika, hivi sasa TEF tunafuatilia kwa karibu uhusiano wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, na vyombo vya habari kutokana na matukio ya mara kwa mara ya kudhalilisha wanahabari wanapokuwa kazini kwa amri yake. Matukio haya yakiendelea, tutalazimika kupitia uhusiano wa RC Gambo na vyombo vya habari nchini.
Mwisho, tunavipongeza vyombo vya habari, kwa maana ya magazeti, redio, televisheni na mitando ya kijamii ya ndani na nje ya nchi kwa kutekeleza uamuzi wa kumfungia RC Paul Makonda kwa uaminifu na uadilifu wa hali juu, licha ya vishawishi vya hapa na pale vinavyotolewa na wapambe wake. Nguvu yetu ipo katika umoja wetu kama wanahabari. Tusipoteze. Mungu ibariki Tanzania.
Deodatus Balile
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
Mei 19, 2017
Sitanii, tamko hili tuliliweka kwenye mitandao ya kijamii. Baada ya kuliweka limesambaa kama moto wa pori. Nimepokea simu ya Mkurugenzi wa Sahara Media, Samwel Nyalla, na baada ya muda mfupi nikapokea simu ya Mwenyekiti Mtendaji wa Sahara Media, Dk. Anthony Diallo, siku ya Ijumaa. Waliyoniambia sitayamwaga hapa, ila yamenithibitishia kuwa kipindi hicho kitarushwa.
Moja tu, ambalo nawiwa kulisema, ni kauli yao kuwa “hawaingilii uhuru wa uhariri, hivyo kama wahariri wao wameamua kurusha kipindi hicho, hiyo ni hiyari yao.” Hii niliipenda, na sikutaka kueleza alichosema Dk. Diallo, ila baada ya andiko lake dhidi yangu aliloweka kwenye kundi la WhatsApp la UVCCM Mwanza, likasambazwa katika makundi mengi, nawiwa kufungua pakacha japo kiduchu. Nitaliweka hapa chini.
Diallo ameniambia tamko letu ni kama limewashinikiza, yeye si mwanahabari, hivyo madai ya “Umoja wa Kitaaluma (Professional Solidarity) hayamhusu”. Akanihakikishia kuwa Sahara Media ni kampuni huru, na kipindi hicho kingerushwa. Nilimwambia hilo tulilijua tangu enzi za ujana wetu na yuko huru kumpa nafasi Makonda au yeyote awaye hata kama ni kwa siku nzima.
Ujumbe wa Diallo
Baada ya kupata ujumbe huu nimempelekea Diallo nikimuuliza iwapo tumefika kiwango hiki cha kuchafuana, naye hakunijibu. Katika ujumbe huu Diallo anataka kuiaminisha jamii kuwa TEF inatumwa na upinzani kupinga unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari. Amesema anafahamu historia ya Balile na [Neville] Meena “wanajulikana kuwa mikononi mwa wanasiasa wakubwa wa upinzani.”
Andiko hili la Diallo limeendelea kusambazwa na watu mbalimbali akiwamo Jerry Muro, aliyeniletea maandiko mengi tu yenye tuhuma nitakazoziweka hapa chini pia. Nyingi kati ya tuhuma hizo ni kuwa TEF haitetei maslahi ya wanahabari, haiwaaliki kwenye semina, haitetei walipwe mishahara mizuri na kupewa mikataba ya ajira.
Sitanii, naomba kutangaza maslahi. Mimi na Manyerere Jackton, tunamiliki Gazeti la JAMHURI. Ninao uthubutu wa kusimama nikasema hatudaiwi mshahara/malipo, iwe kwa mwajiriwa au correspondent. Wafanyakazi wa kampuni yetu, wote wana mikataba na mishahara inalipwa kwa mujibu wa makubaliano.
Si mishahara tu, nasema hata michango ya NSSF, Workers Compensation Fund (WCF), Pay As You Earn (PAYE), Skills Development Levy (SDL), Presumptive Tax (Provisional/Corporate Tax), Value Added Tax returns… nazo hatudaiwi kama mwajiri. Kwa sasa tunamalizia mazungumzo na National Health Insurance Fund (NHIF) kwa nia ya kuanza kuwapa wafanyakazi wote wa JAMHURI Media Limited, Bima ya Afya.
Mimi natokea TEF, nikiwa huko TEF mara zote nahimiza haya yafanywe kwa wanahabari na nimeamua kuyafanya kwa vitendo. Nathubutu kusema kama yupo mfanyakazi anayelidai JAMHURI katika hayo ya kisheria niliyoyataja, basi ajitokeze tena bila kuja hapa kwetu, atangaze madai yake kupitia mitando ya kijamii nasi tumlipe. Tunajiendesha kwa shida, ila kimaadili (morals) tunatimiza wajibu na misingi ya kisheria.
Nitafurahi ikiwa na Dk. Diallo, “mtetezi wa uhuru wa uhariri” akijitokeza hapa na kusema kifua mbele katika miaka miwili iliyopita amelipa mishahara mara ngapi? Michango ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya wafanyakazi wake anachangia mfuko upi, mara ya mwisho alichanga lini, kodi za Serikali kati ya nilizoorodhesha amezilipa kwa kiwango gani. Huo ndiyo uzalendo. Hapo ndipo tunaonesha kweli tunajenga nchi, badala ya kutumia maneno chepechepe ya kisiasa kudai Balile na Meena wanashikiliwa na wapinzani, hivyo TEF inatumika.
Umbea wa Jerry Muro
Kutumwa ni kubaya. Mara zote nimesema heri kuishi siku mbili kama simba, kuliko kuishi siku 100 kama nzi. Jerry Muro anashirikiana na wapuuzi wenzake, kututungia tuhuma za uongo, kwa nia ya kuchafua jina la TEF na viongozi wake; Neville Meena na Deodatus Balile. Anadiriki kusema tulikula michango ya rambirambi za mwanahabari mwenzetu aliyefariki, Simon Kivamo, Sh milioni 4.5, alizotoa Makonda.
Kwanza hii ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu. Nitaweka chini majibu aliyopewa, ila kama kuna mtu alifanya kazi ya kutukuka katika kumuuguza Kivamo, kusimamia michango ya msiba hadi inakabidhiwa, basi ni Thompson Bejamin Kasenyenda. Mtu sifa yake mpe. Alipigania uhai wa Kivamo, ila Mungu akampenda Kivamo zaidi. Muro kusema mke wa Kivamo ataambatana na Makonda Star TV kudai rambirambi, ni uzandiki.
Andiko la Muro na lilivyokanushwa
[20/05 10:32] Muro: Jamani kuna taarifa ile fedha 4.5 milioni ya kusomesha watoto wa marehemu mwandishi mwenzetu Kivamwo iliyotolewa na Makonda haikufika kwa mjane mpaka leo, fedha inasemekana zilikabidhiwa kwa Neville Meena na Balile, sasa sina uhakika na hili naomba mwenye taarifa zaidi atujuze kwanza, kabla ya junatatu (Jumatatu) asubuhi please.
[20/05 10:49] mwintumba: Tupe muda kidogo tulifanyie kazi suala hili. Tunahitaji uthibitisho. Nijuavyo mimi mjane alikabidhiwa pesa zilizochangwa kupitia group la Tasnia ya Habari na group la The Guardian Ltd. Kulikuwa na ahadi kutoka kwa watu mbalimbali akiwemo mwenyekiti wa Moat lakini bado hazijatolewa. Tutapa[ta] ukweli kuhusu mchango wa Makonda leo hii.
[20/05 10:50] Angella Michael: Jerry muro na wengine, mimi ndie nilipewa pesa na makonda tena alinikabidhi mkewe osterbay na nikapeleka bank pale coco beach, kwa hili umecopy na kupaste utumbo.nakushauri futa hoja hii.
[20/05 10:53] Angella Michael: Tusipende kuchafuana hata kama hatuna mahusiano mazuri, kwanza anayetakiwa kuongelea kuhusu kivamwo ni wale tuliokuwa wafanyakazi na wafanyakazi mpaka sasa wa guardian ambayo kwa miaka miwili tulikuwa tukichanganishana pesa za matibabu zake na hata chakula kwa familia yake na kwa kushirikiana na wadau.
[20/05 10:53] Angella Michael: Hawa kina nevile na wenzake wasulubiwe kwa mengine kwa hili waombeni radhi.
[20/05 10:55] Angella Michael: Narudia tena hata kama tunachukiana tusifikie hatua ya kuchukiana si tabia nzuri, nevile na balile leo niachieni hii kesi nitainunua.
Sitanii, ni kwa sababu ya nafasi tu nimefupisha mjadala ulioendelea. Asante dada Angella. Jerry amenitumia ujumbe huo kwenye simu yangu, ila kwa kuuchezea kidogo akaondoa jina langu, kwenye makundi mengine akaweka jina langu. Najiuliza, nini hiki kimetokea hadi tunafikia kutungiana uongo mkubwa kiasi hiki hadi mtu anaumbuliwa na wenye kuujua ukweli?
Jerry Muro, mdogo wangu, naomba kukushauri njaa uiache iendelee kubaki tumboni, ukiiendekeza ukairuhusu ikaingia kichwani hadi ukatoa fikra za hivi, jamii itakushangaa mno.
Naomba kuchukua fursa hii kusisitiza mambo mawili ya msingi. TEF, Balile au Meena hawana ugomvi binafsi na Makonda au Serikali. Tunachokifanya ni kulinda heshima ya taaluma yetu. Zipo taasisi za kihabari ambazo kazi yake imekuwa ni kutoa matamko ya pongezi, semina na wakati mwingine kusemea waandishi wa habari zikiwa kwenye viyoyozi. TEF iko ‘newsroom’. TEF imevaa kiatu inafahamu fika panapouma.
TEF inapotetea uhuru wa wanahabari, maana yake inatetea ustawi wa tasnia nchini na matokeo yake itakuwa huduma bora. Mwandishi wa habari akiandika habari ametulia, matunda yanaonekana. Mfano hai, sisi Gazeti la JAMHURI tulipoandika habari ya Kampuni ya Lake Oil kukwepa kodi kupitia mafuta ya transit, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilichunguza, ikambana Lake Oil akalipa Sh bilioni 8.5 kama kodi aliyokuwa amekwepa.
Hii kwetu ni faraja kubwa. Magazeti, radio, televisheni na mitandao ya kijamii mingi imelinufaisha Taifa hili kwa kuweka wazi uozo na nchi ikaokoa mabilioni. Hivi, kama si vyombo vya habari fedha za EPA, Kagoda, Meremeta, East Africa Power Limited, Mecco, Escrow na mengine mengi yangefahamika? Tungejua bandari kuwa wanatumia kijiti bila ‘flow meters’ tangu mwaka 2011 hadi 2015?
Sitanii, TEF na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kuwa wanachama wake wako ndani ya vyumba vya habari wanayaona na kuyaishi haya. Wanafahamu mwandishi wa habari anapokwazwa, uhuru wake unapoingiliwa na mtu kwa kwenda chumba cha habari na mitutu ya bunduki, kisha akashinikizwa atangaze habari aitakayo mkubwa yule, basi nchi haitanufaika na uandishi.
Naomba kuazima mfano wa Prof. Issa Shivji. Amepata kusema kuwa mtu asiye daktari, ikitokea akamiliki biashara ya hospitali, hakuna wakati wowote anaoweza kwenda hospitalini akamwamuru daktari aliyemwajiri amdunge aina fulani ya sindano/dawa mgonjwa. Akasema hawafanyi hivyo kwa kuwa hawana utaalamu huo.
Ni bahati mbaya, baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari wasio wanahabari wanatumia kichaka cha umiliki wao kuelekeza wahariri au waandishi wao waandike nini. Najiuliza hii ni dharau, ni ukosefu wa kujitambua kuwa wao si wataalamu wa masuala ya habari au kiburi cha asili cha kudhani kila anayejua kusoma na kuandika anaweza kuwa mwandishi wa habari?
Sitanii, naomba kuhitimisha kama nilivyoanza. TEF, mimi Balile au Meena hakuna mwenye ugomvi na Makonda. Ombi letu kwake ni aiheshimu taaluma ya habari. Ni wazi anafahamu umuhimu wa waandishi wa habari na ndiyo maana anaitafuta Star TV. Kutoka RC aliyekuwa anapata vinasa sauti (microphone) 20 hadi 50 akiitisha mkutano hadi kufikia microphone 1 au 2, ni lazima Makonda apate msongo wa mawazo.
Narudia, sina uhakika kama hadi naandika makala hii, sina kama jana angeomba radhi au la, maana makala hii nimeiandika Jumamosi. Ikiwa hakuomba radhi bado fursa anayo. Kwa kaka yangu Dk. Diallo, napenda kumkumbusha ukweli kuwa TEF hatuna nguvu za kidola (statutory powers), lakini tunayo mamlaka ya kimaadili na kitamko (moral and declaratory powers). Kama huamini kuwa vyombo vya habari ni Muhimili wa Nne wa Dola (usio rasmi) muulize Makonda.
Hatuna gereza, mahakama au polisi wa kukamata wanaotutendea makosa sisi wanahabari, lakini tunaamini kwa kumfungia Makonda tangu Machi 22, 2017 hadi leo kuna kitu amejifunza. Nimeona baadhi wanadai asipoangalia anaweza kufutika katika ramani ya siasa. Wengine wanasema tumejipa mamlaka ya kimahakama, ila mimi nasema tunatetea uhuru wa habari kwa wivu wote.
Nasema, Dk. Diallo na wamiliki wengine wa vyombo vya habari mnao wajibu wa kimaadili (moral obligation) wa kulinda mshikamano wa kitaaluma (professional solidarity). Unaweza kudhani umefanikiwa kutugawa, ila najua ulipo unajuta kwa ulichofanya, japo ni kawaida kwa baadhi ya wanaume kujipiga kifua na kujisemea “potelea mbali.” Makonda tuombe radhi yaishe, tusonge mbele. Tuna jukumu la kujenga viwanda badala ya haya makandokando. Mungu ibariki Tanzania.