Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)imepanga kufadhili jumla ya miradi 113 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za msingi na Sekondari kwenye maeneo mbalimbali nchini yenye thamani ya sh.bil.11.3.
Hayo yameelezwa leo Februari 25,2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TEA,Dkt.Erasmus Kipesha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.

Dkt.Kipesha amesema katika kufanikisha hayo, Mamlaka hiyo imetenga bilioni 3.0 kwajili ya kuimarisha miundombinu ya utoaji wa mafunzo ya amali ili kufanikisha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu huku jumla ya shule 20 zikitarajia kunufaika na mpango huo .
Aidha amesema katika kipindi cha miaka minne ya awamu sita,Mamlaka hiyo imepokea jumla ya Sh.bil.49.05 kutoka serikali kuu kwa ajili ya mfuko wa Elimu na jumla ya sh.bil.3.8 kwajili ya mfuko wa kuendeleza ujuzi.

Amesema mradi utakapokamilika utanufaisha wanafunzi 29,482 na walimu 12 katika shule za msingi na sekondari.
“Miradi hii inajumuisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 45 pamoja na ukarabati wa vyumba vya madarasa 11,matundu ya vyoo 336,nyumba za walimu 12,mabweni 8 na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwa shule 9,” ameeleza.

