Na Mwandishi Wetu, Arusha
Katika makala iliyotangulia nilifafanua gharama ya uamuzi wa TCU kwa upande mmoja kuzuia baadhi ya vyuo binafsi, kati yake vimo vile vinavyomilikiwa na taasisi za dini, kutodahili wanafunzi kwa mwaka huu wa masomo na kuzuia baadhi ya kozi zisiendelee kufundishwa.
Tafsiri ya uamuzi huu ni kama vile, leo taasisi binafsi ndiyo chanzo cha kudorora kwa elimu na uwepo wa wahitimu dhaifu nchini mwetu, kitu ambacho si kweli.
Msingi wa watoto wetu kwenye elimu ni dhaifu, ndiyo maana tunashangaa juhudi hizi za TCU kutaka kurekebisha hapa juu ilihali chini wanapoanzia hali ni mbaya.
Walimu ni wachache na pengine hata wasio na sifa, hawalipwi ipasavyo, ufundishaji hafifu, miundombinu haba au imechakaa, mfumo wa upimaji (mitihani ya taifa) usiozingatia uhalisia, kwa maana, shule zisizo na walimu na mazingira bora ya kujifunzia, hasa shule za umma (shule za kata), kufanya mtihani mmoja na shule zenye walimu wengi na mazingira stahiki ya kujifunzia.
Lakini ni ajabu pia, serikali kutizama suala la elimu upande mmoja tu wa KUFAULU MITIHANI na kusahau mambo mengine hata kama yanapaswa kushughulikiwa yote kwa pamoja.
Elimu na tabia ya anayeelimika vinapaswa kwenda pamoja, kikibaki kimoja kati ya hivyo hakutakuwa na faida yoyote kwa jamii. Tena bora kuwa na tabia njema hata kama hujaelimika unaweza kuifaa jamii, kuliko kuelimika ukakosa tabia njema (maadili).
Matokeo yake ni kama haya tunayaona ya ukosefu wa maadili kwa kiwango kikubwa miongoni mwetu. Ni kitambo sasa tumekuwa na harakati za kutafuta majibu ya changamoto ya maadili miongoni mwetu na hasa kwa vijana.
Tumeshuhudia vitendo vingi vya rushwa kati yetu, tamaa ya kutaka kutajirika haraka, wizi wa mali ya umma, udanganyifu, matumizi mabaya ya madaraka, ubinafsi, vitendo vya kikatili na hujuma nyingi mbali mbali.
Hata hivyo, tumeisikia serikali ikitoa wito mara kwa mara, kuwa taasisi za dini zisaidie kuondoa hali ya kukosekana kwa maadili miongoni mwetu, na kwa kweli, taasisi za dini zina nafasi ya pekee kurudisha maadili mema kwa nchi yetu.
Kwa anayetambua madhara ya mkosi huu wa kukosekana kwa maadili, katu hawezi kushawishika kufungia taasisi hizi zisiendelee kutoa elimu na hasa kwa ngazi ya elimu ya juu au kuziwekea vikwazo ili zikose wanafunzi hatimaye zijiondoe kwenye jukumu la kutoa elimu.
Na inavyoonekana, kauli ya Rais aliyoagiza udahili urudi kwenye vyuo ili vyuo vitakavyokosa wanafunzi vifunge vyenyewe, imechukuliwa kwa namna potofu kabisa. TCU inafanya hujuma kwa vyuo binafsi ili vifungwe.
Itakuwa ni kujidanganya na kusubiri janga, kudhani vyuo vya umma pekee vitaleta ufanisi tunaoutaka kwenye elimu. Ni hivi juzi tu, kati ya 2000 – 2006 serikali ilishindwa kabisa kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa na sifa ya kuendelea na elimu ya juu.
Ni vyuo binafsi vingi na hasa vinavyomilikiwa na taasisi za dini vilivyoanzishwa wakati huo, vilisaidia kuondoa kadhia hii. Leo vinafungiwa viondoke kwenye kutoa elimu..! Hata hivyo, Kwa wanaojua ulinganifu wa utendaji kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, sekta ya umma haijawahi kuwa na ufanisi wa kudumu mahali popote, labda Tanzania ndiyo ianze kuwa mfano sasa (The government is inherently inefficient- Ron DeSantis). Itaendelea…