Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es salaam

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wametangaza rasmi Mashindano ya Tuzo za Waandishi wa habari za maendeleo ‘Samia Kalamu Awards’ zenye kauli mbiu ya ‘Uzalendo ndio Ujanja’

Tuzo zenye lengo la kuchochea uandishi wa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na kujenga chapa na taswira ya nchi ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa kutangaza tuzo hizo, leo Oktoba 13,2024 Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben amesema tuzo zitahusisha maudhui yaliyochapishwa kupitia magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni akisisitiza kuwa ni tuzo maalumu kwa vyombo vya habari na maafisa habari wa serikali.

“Tuzo hizi zilizoandaliwa na TAMWA na TCRA zitahusisha habari zilizochapishwa kati ya Januari 1 hadi Oktoba 26,2024. Tuzo hizi zitatolewa kwa wanahabari Watanzania kwa lengo la kuhamasisha, kuhimiza na kukuza wigo wa uchakataji, utangazaji na uchapishaji maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari”,ameeleza Dkt. Rose.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia na utandawazi, uandishi wa habari nchini umekuwa ukijikita kwenye kuburudisha, kuhabarisha huku uandishi wa makala za kuelimisha zikiwa kwa kiwango kidogo lakini pia vyombo vya habari nchini vimekuwa vikitangaza maudhui ya nje yasiyokidhi mahitaji ya hadhira ya Kitanzania.

Na kwa muktadha huo, TAMWA kwa kushirikiana na TCRA tuliamua kutoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari, watangazaji , wahariri,mameneja, maafisa habari, wamiliki wa vyombo vya habari, wahadhiri na watengeneza maudhui wa mitandaoni wapatao 2,054 kote nchini kwa kipindi cha miezi mitatu mwaka huu 2024″,ameongeza Dkt. Rose.

Amefafanua kuwa, pamoja na mafunzo hayo wameona ni vyema kutoa tuzo kwa wanahabari pamoja na vyombo vya habari ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kuandika, kuchapisha na kutangaza maudhui ya ndani hasa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi wenye tija kwa watanzania.

“Tuzo hizi zimepewa jina la Samia Kalamu Awards ili kutambua na kuenzi historia ya kuwa na Raiss wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na zinatarajiwa kutolewa Novemba 2024 zikiwa katika makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalum za kitaifa, Tuzo kwa vyombo vya habari na Tuzo za Kisekta”,amesema Dkt. Rose.

Amevitaja vigezo vya ushiriki kuwa ni Makala zinazoshindanishwa ziwe zinahusu masuala ya maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi na fursa zinazopatikana kutoka kwenye miradi mbalimbali.

Makala hizo ziwe zimechapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza kwenye vyombo vya habari vya ndani au nje ya Tanzania. Aidha mwandishi awe Mtanzania na makala iwe imefanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina. Vyanz vya habari visipungue vinne na makala hazipaswi kuwa zimeshawahi kushindanishwa kwenye tuzo nyingine”,amefafanua Dkt. Rose.

“Kwa kuzingatia ulinzi wa haki miliki, kazi zote zitakazowasilishwa kwa ajili ya mashindano ni lazima ziwe za kipekee na zifuate masharti ya hakimiliki ya mwandishi na kituo kilichotangaza”,amesema.

Amesema mchakato wa upigaji kura utahusisha wananchi kwa asilimia 60 na majaji kwa asilimia 40, kura zitapigwa kupitia SMS SHORT CODE namba 15200 kupitia simu na kutumia tovuti ya https://samiaawards.tz kwa mawasiliano zaidi tembelea tovuti https://samiaawards.tz

“Matarajio yenu ni kwamba Samia Kalamu Awards zitahamasisha uandishi wa habari unaozingatia weledi, maadili, kukuza maendeleo ya Tanzania na uzalendo hivyo kila mwanahabari anatakiwa kutumia fursa hii kuwasilisha kazi kupitia tovuti ya https://samiaawards.tz”,amesema.

Please follow and like us:
Pin Share