Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MKUU wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaja amewataka wananchi kuongeza umakini katika matumizi ya simu za mkononi na mtandao wa intaneti na kutofungua au kutosambaza viunganishi (links) wasivyovijua kwani vinaweza kuwaletea athari.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Amesema baadhi ya watu wamekuwa si waaminifu wanaweza kutumia njia hiyo kupata taarifa ambazo zinaweza kuleta athari kwa muhusika.

“Katika maonesho haya tumetoa elimu kwa wakulima na wadau mbalimbali jinsi ya kujilinda kutokana na changamoto mbalimbali za mtandao, tumewataka wahakikishe hawafungui links wasizozifahamu. Inaweza kuwa kwenye WhatsApp mtu amekutumia links au kiunganishi kwamba shiriki bahati nasibu au sambaza utapata zawadi fulani, usifanye hivyo…link usiyoifahamu usifungue na wala usisambaze,” amesisisitiza.

Vilevile ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuhakiki namba zao za simu kwa sababu suala hilo ni endelevu na kuripoti kwa watoa huduma namba wasizozifahamu ili ziweze kuondolewa.

Amesema ni rahisi mtu kutumia namba ya kawaida kumpigia mtumiaji wa huduma za mawasiliano kutaka kuomba taarifa au kumwambia kwamba ameshinda bahati nasibu wakati si kweli.

“Wananchi wasipokee maelekezo yoyote kwa mtu anayejifanya kwamba ni mtoa huduma, hakikisha mtu ambaye anakupigia na kukupa maelekezo kwamba ni mtoa huduma anatumia namba 100, tofauti na namba 100 usipokee maelekezo,” amesema.

Amesema katika maonesho hayo wamekutana na wadau mbalimbali ambao wamepewa miongozo ya kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka hiyo ambazo mtu anaweza kuhudumiwa kokote aliko kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ambayo ni rahisi.