Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Ripoti ya Utendaji wa Kisekta imeonesha ongezeko la asilimia 3.4 kwa laini za simu zinazotumika,ambapo hadi mwezi Juni 2022 kulikuwa na laini Milioni 56.2 idadi iliyoongezeka hadi kufikia laini milioni 58.1 Septemba 2022.
Takwimu zinaonyesha kwamba mikoa mitano nchini inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya laini za simu zinazotumika yaani (Active SIM-cards) hadi Septemba 2022 ni Dar es Salaam (laini Milioni 9,756,697), Mwanza (laini 3,700,914), Arusha (3,448,200), Mbeya (3,089,848) na Tabora (3,060,407).
Aliyasema hayo Oktoba 25,2022 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Dkt.Jabiri Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema uchambuzi wa laini hizo kwa watoa huduma unaonyesha kwamba kuna ushindani mkubwa kwani hakuna mtoa huduma mwenye zaidi ya asilimia 35 ya laini ya zilizosajiliwa.
“Mwelekeo wa usajili kwa miaka mitano iliyopita unaonyesha ongezeko la asilimia nane kwa mwaka. Kuenea kwa laini miongoni mwa watu kumeongezeka kwa asilimia nne kwa mwaka. Kuenea kulikuwa asilimia 78 mwaka 2017, asilimia 81 mwaka 2018 , asilimia 88 mwaka 2020 na asilimia 91 mwaka 2021”. Amesema
Aidha amesema wastani wa gharama za vifurushi vya simu zilikuwa shilingi 7.8 kwa kupiga simu ndani ya mtandao Septemba 2022, kutoka shilingi 7.7 Juni 2022. Pamoja na ongezeko hili dogo, gharama bado ni chini kulinganisha na vifurushi vya simu kwenda mitandao mingine” amesema.
Amesema wastani wa vifurushi vya simu kwenda mitandao mingine ulikuwa shilingi 8.1 Septemba 2022, ikiwa ni ongezeko kutoka shilingi 7.6 Juni 2022.
Hata hivyo amesema watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka 29,169,958 Juni 2022 hadi 31,122,163 Septemba 2022 sawa na ongezeko la asilimia 6.7.
“Mwelekeo wa ongezeko la watumiaji wa intaneti linaonesha kwamba kulikuwa na ukuaji wa takriban asilimia 17 kila mwaka,katika kipindi cha miaka 5 ambapo mwaka 2017, kulikuwa na watumiaji Milioni 16,106,636 na mwishoni mwa mwaka 2021 waliongezeka kufikia Milioni 29,103,482” ameeleza.
Ameeleza kuwa matumizi ya intaneti yameongezeka kutoka wastani wa MB 6,037, kwa mtumiaji Machi 2022 hadi MB 6,626 kwa mtumiaji Septemba 2022.