Dodoma

Na Mwandishi Wetu 

Kikosi kazi cha kukusanya maoni ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa na ile ya uchaguzi, kimetakiwa kukusanya maoni na mapendekezo ambayo hayataibua maswali kwa serikali wakati wa kuyapitisha.

Agizo hilo limetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa wa Haki, Amani na Maridhiano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Mkutano huo uliofanyika Aprili 5, mwaka huu, jijini Dodoma, ulihudhuriwa na takriban vyama vyote vya siasa vilivyopo nchini, isipokuwa Chadema na NCCR-Mageuzi, vilivyosusa kwa madai mbalimbali.

Katika mkutano huo, Rais Samia ameitaka TCD kujadili na kutoa kwa serikali mapendekezo kwa kuzingatia hali halisi na mazingira ya Tanzania huku akibainisha kuwa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa yatategemea mambo yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo.

Mwenyekiti wa TCD aliyemaliza muda wake, Zitto Kabwe, amesema kwa miaka 10 kituo hicho kimekuwa na utaratibu wa kufanya mikutano ya kuponya majeraha ambayo vyama vya siasa vinayapata kila baada ya Uchaguzi Mkuu.

Zitto amemweleza Rais Samia kuwa yote yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo yatachukuliwa na wajumbe wa kikosi kazi, kwani jukumu lao ni kusikiliza maoni ya wadau wengine na kuyaboresha kabla ya kuyafikisha kwa Rais.