Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
CHAMA cha Wafanyabiashra wa Ng’ombe Tanzania (TCCS), kimesema kinaendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha sekta ufugaji nchini inazidi kuboreshwa na kufanya kuwa ufugaji wa kisasa.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kibiashara wa Ng’ombe(TCCS), Naweed Mulla wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya mifugo na mnada unaotarajia kufanyika Juni 14 -15, 2024 maeneo ya Ubena Estate Chalinze.
Amesema lengo la kuanzisha programu hizo ni kusaidia wakulima na wafugaji kujikwamua kiuchumi wao wenyewe na kuongeza pato la taifa kupitia ufugaji.
Amebainisha kuwa takribani washiriki 300 wanatarajia kuhudhuria maonesho hayo ambayo yatafanyika ndani ya siku tatu katika viwanja hivyo.
Ametoa kwa vijana wengi na wafugaji wapya wanaotamani kuingia katika tasnia hiyo ya ufugaji kushiriki katika maonesho hayo ili kuweza kujifunza mambo mbalimbali juu ya ufugaji na kuona namna gani wataweza kufanya biashara hizo za kilimo.
Amesema maonesho hayo yanania ya kuwezesha Jukwaa Madhubuti la Kitaifa la Wafugaji ,wasindikaji na wadau katika mnyororo wa thamani ya mifugo kutambulika kwa lengo moja la kuendeleza sekta hiyo kwa mbinu bora endelevu za kiuchumi na kimazingira.
”Tamasha hilo lilianzishwa na kuchukua nafasi yake kwa mara ya kwanza mwaka 2022 ambapo kwa mwaka huu linatarajia kufanyiwa maboresho makubwa ambayo yataenda sambamba na utoaji wa elimu ili kutoa msaada kwa jamii namna ya kufuga kwa tija,”alisema na kuongeza
”Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ,rafiki na wezeshi kuhakikisha sekta hiyo inawakwamua wakulima na wafugaji kimaisha na kuhakikisha wanaongeza tija na ubunifu katika shughuli za kilimo,”alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugezi Idara ya Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa Benki ya Kilimo,Mkani Waziri alisema wao kama benki kazi yao kubwa na kutoa maendeleo katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi hivyo wameamua kushirikiana na TCCS kuona namna wanavyoweza kuleta mageuzi katika tasnia ya ufugaji.
Amesema wamekuwa washiriki wakuu katika tasnia ya ufugaji ili kuhakikisha watanzania wanafuga kwa tija na kuweza kupata kipato cha kugeuza maisha yao .”Tunatoa mikopo ya moja kwa moja kwa wafugaji katika kuwawezesha wafugaji ambapo hadi sasa benki imetoa jumla ya Bilioni 38 ya mikopo kwa wafugaji kwa wanufaika wapatao 8688 katika mikoa 21,”alisema na kuongeza
”Tumekuwa tunashirikiana na taasisi nyingine za fedha katika kuchangiza taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi kwa kutoa dhamana ya asilimia 50 hadi 70 kwa mikopo mfugaji anaochukua lengo ikiwa ni kuwainua wafugaji wakitanzania,”alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoani Pwani, Ngobere Msamau amesema kupitia maonesho hayo wanatarajia kupata elimu ya kufanya wazidi kuongeza tija katika ufugaji wa kisasa na kuondokana na ule wa kienyeji.
”Maonesho haya yanatupa kujifunza mambo mbalimbali ya ufugaji wa tija na waasili na kuona namna gani wenzetu walivyopiga hatua katika ufugaji bora,” amesema.