Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Timu ya Kitengo Cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma ya Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), ikiongozwa na Meneja wa taasisi hiyo Bw. Matina Nkurlu, imetembelea na kujionea hatua za mwisho za ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za TCCIA kufuatilia kwa ukaribu fursa za uwekezaji kwa wanachama wake na kuimarisha uhusiano na miradi mikubwa ya kimkakati nchini.

Timu hiyo ilipokelewa na Bi. Cathy Wang, Meneja Mkuu wa EACLC na Mdau mkubwa na mwanachama wa TCCIA, ambaye alielezea maendeleo ya mradi huo ambao umefikia kiwango cha zaidi ya asilimia 95 ya ujenzi. EACLC ni mradi wa kisasa wenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 110 ukiwa umesajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, na unatarajiwa kukamilika rasmi Julai 2025.

Akizungumza katika ziara hiyo, Bw. Matina Nkurlu alieleza kuwa TCCIA inapongeza dhamira ya mradi huo wa kimkakati katika kuimarisha biashara na ajira. “Ni jambo la kufurahisha kuona kuwa zaidi ya asilimia 90 ya maduka hapa yatamilikiwa na Watanzania, jambo linaloashiria mwamko mkubwa wa Watanzania katika kushiriki uchumi wa kisasa,” alisema Nkurlu.

Naye Afisa Uhusiano wa soko hilo, Bi. Saburinq Komba alisema EACLC litakuwa soko kubwa la kimataifa la bidhaa za jumla, likiwa na zaidi ya maduka 2,000, maeneo ya ofisi, maegesho ya magari zaidi ya 1,000, na huduma nyingine za kisasa kama mifumo ya usimamizi wa biashara, Usalama wa saa 24, na miundombinu rafiki kwa biashara za ndani na nje ya nchi. Mfumo wa uendeshaji wa soko hili umechukua mfano kutoka masoko maarufu ya Yiwu na Guangzhou nchini China, Alieleza Bi. Komba.

Kwa upande wake, Bi. Wang alibainisha kuwa EACLC litaunganisha moja kwa moja wazalishaji na wafanyabiashara wa China na wale wa Tanzania, na kuvutia wanunuzi kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki. “Tunaunda daraja la kibiashara kwa ukanda mzima. Hili si tu ni fursa kwa Tanzania, bali ni nguzo mpya ya biashara ya kikanda,” alisema Bi. Wang.

Kupitia ziara hii, TCCIA imethibitisha tena nafasi yake kama daraja muhimu linalowaunganisha wanachama wake na miradi ya maendeleo, ikiendelea kuhamasisha sekta binafsi kuchangamkia fursa za kimkakati kama EACLC kwa ajili ya ustawi wa biashara na ukuaji wa uchumi wa taifa.