Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

WAKULIMA na wadau wa mbalimbali wametakiwa kuhudhuria mafunzo pamoja na kuwa na leseni ya uendeshaji wa matumizi ya ndege nyuki maarufu (DRONES) badala ya kutumia vifaa hivyo kiholela.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

“Tuko hapa kwenye maonesho ya Nanenane Dodoma kwa lengo kubwa la kutoa elimu kwa umma ili waweze kufahamu shughuli zetu tunazozifanya, kazi zetu lakini pia tunaendesha Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) waweze kufahamu kinafanya nini pamoja na kozi mbalimbali tunazozitoa.

“Sasa hivi kutokana na Teknolojia kukua kumekuwa na utitiri wa ndege nyuki (drones)…sasa ndege nyuki ni ndege na sio wote wanaolifahamu hilo, kwahiyo tumekutana hapa tuwaeleze waweze kuelewa hilo ili anayetumia aweze kupata vibali vya kuendesha hicho chombo, leseni stahiki na wewe mwenyewe kama rubani lazima upate mafunzo stahiki na lazima ujue kanuni za kianga ili uweze kutumia hicho chombo,” amesema na kuongeza:

“Ndege nyuki sio kamera, ndege nyuki ni ndege kama zilivyo ndege zingine huwezi kuirusha angani bila kutoa taarifa na bila kujua uko wapi ili sisi tuweze kuwataarifu Wanaanga wengine kwamba kuna mtu yuko maeneo fulani anarusha ndege nyuki kwani ikifyonzwa na ndege zinazoruka zinazobeba abiria inaweza kusababisha ajali,” amesema Johari.

Akizungumza kuhusu Chuo cha Usafiri wa Anga, amesema amesema tayari wameshapata fedha kutoka serikalini za kuanza ujenzi wake.

“Tunaendesha mradi wa Chuo cha Usafiri wa Anga ambapo kinafundisha mafunzo ya Anga lakini kina dahili wanafunzi wa kitanzania na kimataifa..kwahiyo ni chuo ambacho kinaingizia serikali fedha za kigeni. Lakini tulikuwa na changamoto ya kutokuwa na majengo mahususi kwaajili ya chuo, kwahiyo tukasema tuanze mikakati ya kujenga chuo cha kisasa.

“Tumeomba serikali tayari tumepata ardhi, michoro imekamilika na gharama ni kiasi cha Sh. Bilioni 78. Kwa mwaka jana serikali ilitenga kiasi cha Sh. Bilioni 5 na kwa mwaka huu wa Fedha imetenga Sh. Blioni 25…kwahiyo kwa fedha hizo tunaanza utekelezaji wa mradi na tayari tumeshapata Mshauri Mwelekezi,” ameongeza.

Naye Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), Aristid Kanje amesema kwa kuwa chuo hicho ni cha kimataifa, wameshiriki maonesho ya Nanenane kuweza kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zilizopo katika sekta hiyo.

“Tukaona kushiriki maonesho haya kwasababu kuu tatu, ya kwanza tukijua sekta ya anga ndio chachu ya uchumi wa nchi yoyote, pia kuwaeleza wananchi fursa zilizopo katika usafiri wa anga, tukiwaleta vijana kupata mafunzo wanaweza kupata ajira ndani ya taifa na nje ya taifa.

“Pia kuwaelimisha wananchi hasa Wakulima wetu wajue namna bora ya kutumia ndege nyuki katika kuboresha kilimo. Tunaenda na Teknolojia ambapo akitumia drones ikiwa ni kwaajili ya kufanya ukaguzi wa shamba lake kujua sehemu ya kuweka dawa kwaajili ya kuweka mbolea itamfanya ataweza kufanya kilimo kuwa rahisi, gharama nafuu na chenye tija,” amesisisitiza.

Please follow and like us:
Pin Share