*Wakurugenzi wahariri Waraka wa Hazina
*Mbinu hiyo yawafanya walipane mamilioni
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), inakabiliwa na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Fadhil Manongi, hadi wiki iliyopita bado alikuwa akiendelea na dhima za kiofisi licha ya muda wake wa kung’atuka kuwadia.
Wakati Manongi akijiandaa kuiacha ofisi hiyo, kumekuwa na malalamiko ya matumizi mabaya ya fedha miongoni mwa wakurugenzi ambao ni washirika wake.
Ni kwa mtiririko huo, Mkurugenzi Mkuu huyo amehakikisha mikataba ya wakurugenzi kadhaa inahaririwa ili kukidhi matakwa ya kisheria ya kuwapatia nyumba, licha ya Waraka wa Msajili wa Hazina kuagiza vinginevyo.
Waraka huo wa Julai 22, 2010 katika kipengele namba 3 unasema, “Madhumuni ya waraka huu ni kuainisha utaratibu mpya wa malipo ya posho ya nyumba kwa viongozi na watendaji wakuu wa taasisi za Serikali, ambao masharti yao ya kazi ni pamoja na kupatiwa nyumba ambayo hawatalipia pango, lakini taasisi zimeshindwa kuwapatia nyumba.”
Kwa maelezo hayo, wakuu wa taasisi za Serikali posho yao ya nyumba kwa mwezi ni Sh 800,000; ilhali wakuu wa viidara na vitengo kwa watumishi wenye ngazi za mshahara za PUT/PHTS/PGMS/PRSS 18-21 ni Sh 600,000 kwa mwezi.
Baada ya kuupata waraka huo, Mkurugenzi wa Utawala, R. Ruhongole, Agosti 10, 2012 alimwandikia barua Manongi akiomba baraka za kufanywa kwa marekebisho ya nyongeza kwenye mikataba ya wakurugenzi na wakuu wa vitengo husika ili waweze kupata posho hizo.
Ruhongole aliandika, “Kama ilivyozungumzwa kwenye kikao cha EMT cha Agosti 7, 2012, mameneja na machifu ni wasaidizi wakuu wa wakurugenzi. Kwa kuwa matakwa ya Waraka Na. 3 wa mwaka 2010 unataka walipwaji wa posho hiyo, barua zao za ajira/uteuzi ziwe zimeainisha kama moja ya stahili, nashauri wahusika wote wapewe ‘addendum’ (marekebisho) ya barua zao za ajira kuainisha kipengele hicho.
“Hatua hii itatosheleza kuondoa manung’uniko ambayo yanaweza kuzorotesha utendaji kazi…naomba uridhie ili waweze kulipwa kuanzia Julai 1, 2012 ambao ndiyo mwaka ambao bajeti imetengwa.”
Kwa matinki hiyo, vigogo waliowezeshwa kulipwa posho hiyo ni Placid Kauzeni (Mkaguzi Mkuu wa Ndani), Said Kaswela (Meneja Ununuzi), Magesa Sarota (Meneja Ubora wa Bidhaa), Bestina Magutu (Ofisa Habari), Anthony Makwaia (Ofisa Mipango Mkuu), na Margareth Kyarwenda, ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Anga.
Wengine ni Kapteni Michael Mnyune, Julius Kamhabwa, Saidi Onga, Valentina Kayombo, Said Mteule, Viola Masako, Daniel Malanga na Rodney Chubwa.
Kwa upande wake, Manongi ametetea uamuzi wa uongozi wake “kuhariri” mikataba ya watumishi hao ili walipwe posho za nyumba kwa maelezo kwamba ndivyo Waraka Na. 3 wa Msajili wa Hazina ulivyotaka.
“Tulipoboresha ni pale tulipotakiwa na Waraka wa Hazina, nashangaa unalileta hili hapa,” amesema Manongi.