Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Shehena ya bidhaa mbalimbali vikiwemo vipodozi vyenye viambata vya sumu zenye uzito wa tani sita zimeteketezwa baada ya kuondolewa sokoni kutokana na kutokidhi matakwa ya viwango.
Bidhaa hizo zimeteketezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika dampo ya Buhongwa Jana, jijini Mwanza baada ya kukamatwa kwenye mikoa sita ya Kanda ya Ziwa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uteketezaji wa bidhaa hizo, Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Brown alitaja bidhaa zilizoteketezwa mbali vipodozi vyenye viambata vya sumu kuwa ni pamoja vyakula vilivyokwisha muda wa matumizi.
Kwa upande wa vipodozi vilivyoteketezwa, Brown alisema vilipigwa marufuku kutumika nchini kutokana na kuwa na madhara ya kiafya kwa watumiaji ikiwemo kusababisha kansa.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa shirika la viwango Tanzania pale wanapokumbana na bidhaa wanazotilia mashaka vikiwemo vipodozi vilivyozuiwa katia soko la Tanzania, kwani shirika hilo lipo kwa ajili ya kulinda walaji na kuhakikisha wanapata bidhaa kulingana na thamani ya fedha zao
Aidha, alitoa mwito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuangalia muda wa mwisho wa matumizi kwenye vifungashio vya bidhaa wanazotaka kununua ili kuepuka kununua bidhaa zilizoisha muda wake wa matumizi ambazo zinakuwa na madhara kiafya.